Kelvin John bado kidogo Stars

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga klabu ya Aalborg BK ya Denmark, Kelvin John amekingiwa kifua na wadau mbalimbali, huku wakihoji ni kwa nini haitwi timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Mshambuliaji huyo kabla ya kujiunga na Aalborg aliichezea Genk ya Ubelgiji alikoitumikia pia nahodha wa Stars, Mbwana Samatta.

Kelvin amekuwa na mwanzo mzuri tangu alipojiunga na klabu hiyo akicheza mechi saba kwenye mashindano mbalimbali na kufunga mabao matatu.

Kocha wa Alliance, Ezekiel Chobanka alisema Kelvin ni mshambuliaji mzuri na kufunga sio jambo la ajabu kutokana na ubora wake wa kuliona lango.

“Ishu ya kuitwa Stars ni nyingine kwa kuwa kocha ndiye anajua amtumie nani kulingana na mechi, lakini kwangu mchezaji kama yeye ni msaada mkubwa kwa Stars kutokana na uhaba wa washambuliaji katika eneo hilo,” alisema Chobanka.

Kocha wa zamani wa JKT, Ally Ally alisema ni mchezaji mzuri lakini Taifa litamfaidi kama atapata mechi nyingi.

“Hakuna asiyefahamu kiwango chake lakini akipata muda nmwingi wa kucheza kwenye klabu yake naamini atafunga sana na ataleta ushindani kwenye kikosi cha Stars ambacho eneo la ushambuliaji limekuwa na shida kidogo.”

Nyota huyo maarufu ‘Mbappe’, aliishia kucheza mchezo mmoja tu wa ushindani akiwa na kikosi cha kwanza cha KRC Genk, alitumika mara nyingi katika timu za vijana kutokana na ufinyu wa nafasi kwa wababe hao hadi mkataba wake ulipofikia ukomo.

Klabu hiyo kwa sasa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo maarufu kama NordicBet Liga kuanzia 2023 hadi 2024 baada ya kushuka daraja kutoka Denmark Superliga msimu wa 2022-23.

AaB ilianzishwa Mei 13, 1885 na wahandisi wa Kiingereza waliokuwa wakijenga mfumo wa reli wa Jutland na miaka ya kwanza ilijikita kwenye mchezo wa kriketi.

Hapo awali iliitwa Aalborg Cricketklub (Klabu ya Kriketi ya Aalborg) lakini jina la klabu hiyo lilibadilishwa na kuwa Aalborg Boldklub (Aalborg ballclub) mwaka 1899 ndipo soka likaanza kuchezwa.

Tangu wakati huo, ndiyo ukawa mchezo mkuu katika klabu hiyo. Mwaka 1995 AaB iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Denmark kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na ilibata bahati hiyo baada ya Dynamo Kyiv kutupwa nje ya michuano hiyo baada ya kujaribu kupanga matokeo.

Related Posts