UKISIKIA mkwara basi ndio huu. Pamoja na kikosi cha Yanga kuonekana kuwa tishio hasa baada ya kucheza mechi saba tofauti za kimashindano na kufunga jumla ya mabao 24 na yenyewe kuruhusu bao moja, KenGold haijashtuka na kudai watetezi hao wa Ligi Kuu wanafungika tu wakati wanajiandaa kuwapokea.
Yanga iliyotoka kuifumua CBE SA ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 7-0 katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutinga makundi, inatarajiwa kuwa wageni wa KenGold keshokutwa Jumatano jijini Mbeya, huku wenyeji wakiwa na hali mbaya kutokana na kupoteza michezo minne mfululizo iliyopita.
Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Jumanne Challe amesema licha ya ugumu wanaopitia kwa matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu, lakini lolote linawezekana kwa kupata ushindi wa kwanza dhidi ya Yanga.
KenGold ambayo ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu, imekuwa katika kipindi kigumu ikipoteza mechi zote nne hadi kufikia kocha mkuu, Fikiri Elias, kuamua kujiuzulu.
Timu hiyo ilianza ligi kwa kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Singida Black Stars, kisha ikalala 2-1 mbele ya Fountain Gate, ikafa bao 1-0 kwa KMC na juzi ikalala 2-0 ilipoumana na Kagera Sugar na kusalia mkiani.
Jumatano hii timu hiyo itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya utakaokuwa mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana katika historia za klabu hiyo.
Challe ambaye ameipandisha Ken Gold, alisema licha ya ugumu walionao kwa sasa lakini lolote linaweza kutokea akielezea kuwa amewaona Yanga na wanaenda kujipanga kujiuliza na dakika 90 zitaamua.
Alisema baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar wanarejea kwenye uwanja wa mazoezi kujiandaa upya na kufanyia kazi upungufu kuhakikisha michezo inayofuata wanafanya vizuri na kujinasua mkiani.
“Kwa ratiba ilivyo tunamkaribisha Yanga, hatujapata mabadiliko, lolote linawezekana, huu ni mpira niliwaona mechi yao dhidi ya CBE tutaona namna ya kuwadhibiti ili tuweze kupata ushindi na kujiweka pazuri,” alisema kocha huyo.
Yanga imecheza mechi moja tu ya Ligi Kuu na kupata ushindi ugenini dhidi ya Kagera Sugar, lakini imeshinda mechi nne mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 17-0 mbele ya Vital’O ya Burundi iliyoipiga 4-0 na 6-0 mtawalia kisha kuizima CBE kwa 1-0 na 6-0 mtawalia na kutinga makundi kwa msimu wa pili mfululizo, huku pia imeshinda mechi mbili za Ngao ya Jamii 1-0 dhidi ya Simba na 4-1 dhidi ya Azam.