Kiluvya kutumia maujanja ya Yanga

WAGENI wapya wa Ligi ya Championship msimu huu Kiluvya United ya mkoani Pwani, imetamba kufanya vizuri huku ikiweka wazi imefanya maandalizi ya kutosha kuleta ushindani kwa kutumia mbinu za mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara timu ya Yanga.

Katibu mkuu wa timu hiyo, Amri Bashiru alisema, licha ya ugeni wao katika Ligi hiyo ila wapinzani wao wasiwachukulie poa huku akiweka wazi michezo ya kirafiki waliyocheza hasa ule wa Yanga waliopoteza mabao 3-0, umewapa matumaini makubwa.

“Tumepata michezo mingi ya kirafiki na nikiri tu wazi kwamba imetuimairisha, licha ya kupoteza mbele ya Yanga ila kwetu kuna vitu vikubwa tumejifunza kuanzia namna ya kumkabili mpinzani wenye wachezaji bora zaidi yetu,” alisema Bashiru.

Bashiru aliongeza, licha ya kutoweka wazi nyota wapya na wazoefu kama timu nyingine zilivyofanya ila watarajie kukutana na sapraizi kubwa uwanjani, kwani viongozi wamefanya usajili mzuri ambao utashtua wengi tofauti na wanavyowachukulia.

Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi ya Championship msimu huu, imepanda daraja baada ya kuonyesha uwezo mkubwa na kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita katika Ligi ya First League nyuma ya mabingwa wa michuano hiyo African Sports ya Tanga.

Related Posts