MAANDAMANO CHADEMA: Polisi Dar yakamata waandishi wawili wa Mwananchi

Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam wamewakamata waandishi wa habari wawili wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa nyakati tofauti wakati wakiripoti maandamano ya amani yaliyoitishwa na Chadema. Hata hivyo, mmoja ameshaachiwa.

Mpaka sasa jeshi hilo linamshikilia Lawrence Mnubi ambaye ni mpiga picha jongefu (videographer) wa Mwananchi, aliyekuwa eneo la Msimbazi akitimiza wajibu wa kuhabarisha umma, akiwa na kitambulisho na vifaa vya kazi.

Asubuhi ya leo Jumatatu Septemba 23, 2024, mpigapicha wa Mwananchi, Michael Matemanga alikamatwa na polisi eneo la Buguruni, naye alikuwa akitimiza wajibu wake. Aliachiwa baada ya Mwananchi kufuatilia.

Septemba 11, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kufanyika maandamano ya kulaani matukio ya watu kutekwa na kuuawa, akiwemo aliyekuwa kada wake, Ali Kibao. Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime lilitangaza kuyapiga marufuku.

Kwa mujibu wa Mbowe, wameamua kuweka mkazo wa suala hilo, baada ya maombi ya mahitaji, ikiwemo kutaka kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, viongozi waandamizi wa ulinzi na usalama kama sehemu ya uwajibikaji.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi

Related Posts