Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, huku raia wakiendelea na majukumu yao ya kila siku.
Baadhi ya maeneo Wilaya ya Ilala, askari hao wameweka kambi katika baadhi ya vituo, wakiwa na magari ya kuwasha na silaha.
Leo Jumatatu Septemba 23, 2024, saa 12 asubuhi Polisi wameweka kambi eneo la Tabata Barakuda, Vingunguti machinjioni na wengine walionekana eneo la Buguruni mataa.
Kundi lingine liliweka kambi eneo la Buguruni Malapa na askari walionekana kuranda randa kuzunguka eneo hilo, huku wakiwa na silaha. Kambi nyingine imewekwa Ilala Boma na katika mataa ya Karume sokoni.
Hali ni tofauti katika eneo la Kariakoo, kwani askari waliovalia sare, kofia ngumu, wakiwa na silaha wameonekana kutanda maeneo yote, huku wakitembea kwa miguu.
Hata hivyo, wananchi wa kawaida wameonekana wakiendelea na shughuli zao za kila siku, huku baadhi yao wakisema kuna upungufu wa watu ikilinganishwa na siku nyingine.
Mwananchi Digital imeweka kambi katika soko hili kubwa Tanzania ambapo kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 2 baadhi ya maduka yakiwa hayajafunguliwa.
Mmoja wa wafanyabiashara eneo la Kariakoo, Osward Mbilinyi amesema maduka mengi hayajafunguliwa.
“Inawezekana wengi leo watapumzika, maana maduka mengi bado yamefungwa. Labda wengine wanasubiri kukuche vizuri ndiyo wake kufungua, lakini muda kama huu maduka huwa yanakuwa wazi tayari,” amesema Mbilinyi.
Mama Stewart, anayefanya biashara ya mama lishe, amesema kwake leo biashara si nzuri kutokana na upungufu wa wateja.
“Muda kama huu tayari nakuwa nimeuza bakuli hata 15 za supu, lakini leo naona mambo kidogo magumu, labda wanaohofia haya maandamano wateja wangu wengi hawajafungua biashara zao,” amesema Mama Stewart.
Aidha, wananchi wa kawaida wameonekana wakitembea huku na kule na idadi ndogo walionekana wakiingia ndani ya eneo la maduka ya Kariakoo.
Ulinzi huo unatokana na maandamano ya maombolezo na amani yaliyoitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kupinga matukio ya utekaji na mauaji ya wanachama wake na wananchi.
Msingi wa maandamano ni tukio la Septemba 6, 2024 la aliyekuwa kiongozi wao, Ali Kibao kutekwa na watu wasiojulikana akiwa ndani ya basi eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam wakati akielekea mkoani Tanga, kisha mwili wake ukaokotwa umetumwa Ununio.
Maandamano hayo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe yana njia mbili. Ya kwanza ni kuanzia Ilala Boma hadi Mnazi Mmoja na ya pili kuanzia Magomeni hadi Mnazi Mmoja.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Tanzania lilitangaza kuyapiga marufuku maandamano hayo na kusisitiza atakayekaidi hatua kali zitachukuliwa.