Lindi. Makandarasi 42 wamesaini mikataba ya ujenzi wa barabara chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) katika Mkoa wa Lindi.
Hafla ya uwekaji saini imefanyika leo Jumatatu Septemba 23, 2024 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, ikihusisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack amewataka makandarasi hao kufanya kazi kwa mujibu wa mikataba yao.
Amesema wanapaswa kutambua kuwa wamejifunga na dhamana ya kuzifungua barabara hizo zitakazosaidia kuwawezesha wananchi kuzitumia kwa lengo la kuimarisha uchumi wa mkoa huo na ile ya jirani.
Telack amesisitiza kuwa wananchi wana matarajio makubwa, hivyo amewataka makandarasi hao kuhakikisha barabara zinakamilika kabla ya mvua kuanza Desemba.
“Tuna muda mfupi, huu ni mwezi wa tisa, kuna mwezi wa 10 na 11, na mvua zinaanza mwezi wa 12. Nendeni saiti mkafanye kazi, ili wananchi wapate barabara zitakazowezesha kufungua uchumi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Pia amewaagiza wasimamie na kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati, huku akiwataka kuwa makini na kuzingatia ubora wa kazi zao.
“Makandarasi watakaofanya kazi vizuri watapewa kazi tena, lakini wale watakaofanya vibaya hawatapata kazi tena,” amesisitiza.
Akizunguza baada ya kusaini mkataba, Mkurugenzi wa kampuni ya URM Investment, Mwanahamisi Ngalemwa amesema wamejipanga kufanya kazi kwa weledi na bila kupoteza muda.
“Naamini hakuna mkandarasi atakayeshindwa kufanya kazi kwa sababu Serikali imetoa fedha, hata za sisi kukopeshwa na benki ili tukamilishe kazi tunazofanya kwa wakati,” amesema Ngalemwa.
Naye mkandarasi, Godfrey Lukanga wa kampuni ya MR amesema kampuni yake ina vifaa vyote na watahakikisha kazi zote zinakamilika kwa wakati.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Tarura Mkoa wa Lindi, Filbert Mpalasinge amesema mwaka wa fedha 2024/2025, wamepangiwa bajeti ya Sh27.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara, madaraja na usimamizi wa miradi.
“Kati ya mikataba yote 85 iliyopangwa kusainiwa, mikataba 42 ya thamani ya Sh11 bilioni imesainiwa leo,” amesema Mpalasinge.