Arusha. Serikali imewapa kibarua maofisa uhusiano ya umma katika ukanda wa Afrika Mashariki kukabiliana na ongezeko la habari potofu, hasa kwenye mitandao ya kijamii zinazosababisha taharuki.
Ili kufanikisha hilo, imewataka maofisa hao kukumbatia mapinduzi ya kidijitali, hususan matumizi ya teknolojia na Tehama, ili wabaini habari hizo haraka kabla hazijasambaa na kuleta madhara katika jamii.
Hatua hizo zinajumuisha kuziondoa au kuzikanusha taarifa hizo mara moja, ili kuzuia athari zake.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Septemba 23, 2024, jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi wakati wa uzinduzi wa Chama cha Mahusiano ya Umma cha Afrika Mashariki (EAPR).
“Tupo katika zama za mapinduzi ya kidijitali na ni muhimu tutumie teknolojia kusukuma mbele mikakati yetu ya mawasiliano. Msisubiri wengine watumie teknolojia hiyo kuwakwamisha na kuchafua taasisi zenu,” amesema.
Amesema akili mnemba (AI), data kubwa na vyombo vya habari vya kidijitali hivi sasa vinabadili namna watu wanavyopashana habari, kushirikiana na wadau na kupima mafanikio, lakini vina changamoto zake.
Naibu waziri huyo amesisitiza taaluma ya mahusiano ya umma ni nyenzo muhimu ya kujenga imani na kushawishi mijadala ya kijiografia, kuinua ukanda wa Afrika Mashariki, na kuleta mabadiliko ya kudumu duniani kote. “Siku hizi kuna habari nyingi na mifano ni mingi. Ni wajibu wenu kuhakikisha nchi zetu haziingii kwenye taharuki yoyote. Teknolojia inapaswa kuwa msaada wenu katika kuondoa habari potofu,” amesema Mahundi.
Kwa upande wake, rais wa Chama cha Mahusiano ya Umma cha Afrika (APRA), Arik Karani amesema EAPRA ni chombo kipya cha kikanda kilichopewa jukumu la kutangaza Jumuiya ya Afrika Mashariki, watu wake na maendeleo, hasa katika mazingira ya dunia iliyojaa “kelele nyingi.”
“Dunia imejaa mamilioni ya chapa na bidhaa zinazomlenga mtu mmoja mmoja, hivyo kuzidisha kelele. Tumekuja na chama hiki ili kusaidia,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa wa Mawasiliano wa Serikali ya Tanzania (TAGCO), Karim Meshak amesema ana imani Serikali itatenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya EAPRA jijini Arusha.
“EAPRA haitaleta tu mabadiliko bora kwa ukanda huu, bali pia itaboresha jinsi taasisi zinavyowasiliana na kushirikiana katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Meshak.
Amesema kati ya nchi nane za Afrika Mashariki, ni nne tu ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, na Sudan Kusini ndizo zimeunda vyama vya kitaifa vya mahusiano ya umma, huku Sudan Kusini ikiwa bado inakua.
Hata hivyo, Tina Wamala,rais wa Chama cha Mahusiano ya Umma cha Uganda, amesema wako hatua za mwisho za kupitisha muswada wa kutambua taaluma yao nchini Uganda, akibainisha umuhimu wa kudumisha viwango vya kimaadili katika taaluma hiyo.