Mashabiki Yanga wavamia ‘airport’, mastaa wakitua Mbeya

Mbeya. Mashabiki wa Yanga jijini hapa wamejitokeza kwa wingi kuipokea timu yao huku wakitamba kutembeza kipigo kizito watakapoivaa KenGold katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Yanga ambao wametoka kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 7-0 dhidi ya CBE SA, keshokutwa Jumatano Septemba 25 mwaka huu itacheza mchezo wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya KenGold. 

Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa, ambapo wenyeji KenGold hawajashinda mechi yoyote kati ya nne walizocheza, huku Yanga wakicheza mmoja na kushinda dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 2-0.

Wakiwa na msafara wa zaidi ya mabasi sita aina ya Coaster, mashabiki na wanachama wa Yanga walivamia Uwanja wa Ndege wa Songwe kuisubiri timu yao, huku mzuka ukiwa mwingi.

Athuman Likomile ambaye ni mratibu wa Yanga mkoani hapa, amesema KenGold imefungwa sana lakini haijafungwa kwa kishindo, hivyo kazi itaipata rasmi Jumatano.

“Kama tulivyofanya Ligi ya Mabingwa Afrika, naye KenGold atakutana na kipigo cha kishindo, tunajua amefungwa sana ila bado kipigo hajakipata sawasawa, atambue sisi hatukumleta Ligi Kuu,” ametamba Likomile.

Naye Michael Ambilikile amesema matarajio yao ni Yanga kushinda kwa idadi kubwa ya mabao bila kujali KenGold ni ya mkoani Mbeya. 

“Sisi hatujali, tunachohitaji ni kuona Yanga inashinda na tutafunga si chini ya mabao matano, tumekuja mahsusi kuipokea na kuishangilia timu yetu,” amesema Ambilikile.

Related Posts