Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka vijana nchini kuendelea kudumisha Amani, Mshikamano na kuwa na Umoja.
Aidha, amesema vijana ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa maendeleo ya Taifa, hivyo wanatakiwa kuchukua hatua za makusudi kukuza utamaduni wa amani nchini.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo leo Septemba 22, 2024 wakati akizungumza na vijana katika kongamano la kitaifa la Ajenda ya Amani na Usalama kwa Vijana lililofanyika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Center (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani amehimiza vijana kuwa mabalozi wazuri wa amani na kuwa wazalendo kwa taifa lao.
“Niwasihii Vijana kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mabalozi wazuri wa amani ili kuchangia katika kukuza maendeleo ya Taifa letu,” amesema
Naye, Mratibu wa Kongamano hilo la Vijana, Bw. Joseph Malekelea amesema kuwa Kongamano hilo limefanyika kuendana na maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani linalofanyika Septemba 21 kila mwaka lilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kukumbusha watu, mataifa na wadau kuhusu umuhimu wa kudumisha maadili ya amani na usalama.
Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu isemayo “Kijana chukua hatua kufumisha Utamaduni wa Amani Tanzania,”