BEKI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Salford City inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England, Haji Mnoga anakiwasha kwenye klabu yake hiyo mpya na hadi sasa aimeichezea mechi nne.
Mnoga ambaye hakuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kinachocheza mechi za kufuzu Afcon 2025 za Morocco, amekuwa na mwanzo mzuri na kikosi chake hicho kipya akicheza mechi tatu za ligi na moja ya Kombe la FA.
Kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alimwacha Mnoga kwenye kikosi hicho kutokana na kutokuwa fiti, ingawa kwa sasa anapata namba ya kucheza kwenye klabu yake hiyo mpya.
Mnoga akiwa na Stars alikiwasha kwenye michezo mbalimbali ukiwamo dhidi ya Algeria ugenini na kutoka suluhu kwenye michuano ya Afcon ya Ivory Coast mwaka jana na mara ya mwisho aliichezea timu hiyo Machi 22 dhidi ya Bulgaria, mchezo wa kirafiki wa mimataifa.
Kwenye kikosi cha Salford City, tangu atambulishwe Agosti 30 mwaka huu akitokea Aldershot alikodumu misimu miwili tangu ajiunge msimu 2022/23, alicheza mchezo wake wa kwanza wa ligi Septemba 02, dhidi ya MK Dons na kushinda bao 1-0 akitumika kwa dakika 11.
Mchezo wa pili alicheza dhidi ya Wrexham, wakipoteza kwa mabao 2-1 naalicheza kwa dakika zote 90 na Septemba 14 alicheza dakika 34 dhidi ya Cheltenham, Salford ikishinda mabao 2-1 na kuifanya timu hiyo ikusanye pointi nane kwenye mechi tano ikikaa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi kati ya timu 24.