Mwanza. Soko la Machinga la Ukwaju lililopo eneo la Igoma Kata ya Kishiri jijini Mwanza, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya wafanyabiashara 70 na vibanda zaidi ya 3,000, limeteketea kwa moto.
Inadaiwa soko hilo limeteketea leo Jumatatu Septemba 23, 2024 kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 5 asubuhi, huku chanzo cha moto kikidaiwa kuwa ni vijana waliokuwa wakirina asali kwenye moja ya banda lililokuwa na nyuki.
Mwenyekiti wa Mtaa Mbugani, Ally Shija akizungumzia tukio hilo mbali na kudai thamani ya kibanda kimoja ni zaidi ya Sh350,000 ameiomba Serikali kutafuta namna ya kuwasaidia watu waliounguliwa vibanda vyao.
“Muda wa saa nne kasoro tulipokewa simu kutoka kwa uongozi wa wafanyabiashara wa hapa kwamba soko linaungua, niliwajulisha viongozi wangu wa mtaa na watu wa Zimamoto na Uokoaji. Hata hivyo, wakati Zimamoto wanakuja, gari moja lilipata ajali likaja moja.
“Vibanda vilivyoungua hapa ni zaidi ya 3,000 na hatujajua hasara ya mali zilizotekelea, tunaomba Serikali ifikirie hasara iliyotokea na kuona namna ya kutusaidia kwa sababu thamani ya kibanda kimoja kilichoungua ujenzi wake ulikuwa Sh350,000,” amesema Shija.
Akizungumza baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi mbali na kuwapa pole waathirika hao, amedai mabanda yaliyoungua yalikuwa yametelekezwa na wafanyabiashara ambao wamerudi katika maeneo yao ya mwanzo waliyoondolewa.
“Kwa mujibu wa orodha yetu, kulikuwa na wafanyabiashara wasiopungua 2005, lakini kadri siku zilivyokwenda walikuwa wakiondoka na kurudi barabarani… mpaka sasa kwa mujibu wa maelezo ya mwenyekiti wa soko hili na wale ambao tumewasajili kwenye daftari wanakadriwa kuwa 70, kwa hiyo wafanyabiashara wengi walikuwa wameondoka.
“Mabanda yaliyoungua kwa kiwango kikubwa ni ya wale waliojenga na kuondoka, lakini pia yaliyoungua hayakuwa na kitu kwa sababu yalikuwa hayatumiki,” amesema Makilagi.
Hata hivyo, Makilagi amesema ingawa chanzo cha moto hakijafahamika, uchunguzi unaendelea na kuwataka wafanyabiashara hao na wananchi kuwa makini na watu watakaokwenda katika soko hilo na kuanza kupeleka propaganda zenye nia mbaya.
“Viashiria vinaonyesha kule moto ulikoanzia kulikuwa na nyuki kwenye vibanda, kwa hiyo bado uchunguzi unaendelea kufanyika pengine kuna mtu alikuwa anarina asali ndo chanzo cha moto huo kwa sababu hakuna majani wala nyaya za umeme katika eneo lile,” amesema.
Kwa upande wake, mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula amewatoa hofu wafanyabiashara waliounguliwa vibanda na kudai Serikali baada ya kubaini chanzo cha tukio na kufanya tathmini wataona namna ya kuwasaidia.
Ali Mohammed, mmoja wa shuhuda wa tukio hilo amedai awali aliwaona vijana waliokuwa wakirina asali katika moja ya banda lililokuwa na nyuki na baada ya muda mfupi alishangaa kuona moshi na moto ukiteketeza soko hilo.
“Nilikuwa natoka Nyamhongoro stendi narudi nyumbani, sasa wakati napita kule nyuma kwenye banda ambalo lilikuwa na nyuki, kuna vijana walikuwa wamekaa wanakula asali baada mimi kufika pale wakakimbia kuelekea upande wa pili, baada ya kupita lile eneo wakarejea tena.
“Baada kutembea umbali kidogo nikashangaa moto unatokea upande wa juu kule ambako vijana wale niliwaona, kwa hiyo huenda wao ndio chanzo cha moto walivyokuwa wakirina asali,” amesema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na mfanyabiashara mwingine sokoni hapo, Daniel Edward aliyeiomba Serikali kuboresha miundombinu, ili kuepusha majanga zaidi ya moto siku zijazo.
“Hili tukio limetokea asubuhi ya saa 3 na kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda inadaiwa kuna watu walikuwa wanafukuza nyuki kwa moto ndio imetokea majanga kama haya. Naiomba Serikali ituboreshee mazingira, ili ikiwezekana tuendelee na biashara katika eneo hili,” amesema Edward.