Polisi nchini Tanzania yawakamata Mbowe na Lissu – DW – 23.09.2024

Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti, Bara, Tundu Lissu pamoja na watu wengine 14 wamekamatwa na polisi, katikati ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi na wanajeshi wakiwa wametanda katika Barabara kuu za Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.

Maandamano ya maombolezo na amani yaliyoandaliwa na Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania, CHADEMA kufanyika leo Septemba 23, yamegubikwa na taharuki baada ya viongozi wakuu wa chama hicho kukamatwa.

Viongozi hawa wamekamatwa baada ya chama hicho kutangaza maandamano waliyoyaita ya amani yaliyotarajiwa kufanyika Septemba 23 ya kudai ya haki kwa watu waliotekwa na kuuawa wakiwamo makada wa chama hicho.

Mapema hii leo, kulionekana magari ya polisi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ya Buguruni, Ilala, Mnazi Mmoja, Mwenge, Sinza hadi Ubungo na baadhi ya polisi walisimama wakiwa wameshikilia silaha zao.

Tansania | Politiker der Opposition Freeman Mbowe wird verhaftet
Picha: Ericky Boniphace/DW

Awali, hakukuwa na dalili yoyote ya viongozi wa CHADEMA katika maeneo hayo ambayo polisi wametanda lakini kwenye majira ya saa 4 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, DW ilipata taarifa ya kukamatwa kwa Lissu na Mbowe kupitia Wakili wa chama hicho, Hekima Mwasipu.

“Ni kweli chairman amekamatwa amepelekwa central na Lissu amekamatwa yupo kituo cha polisi huku Mbweni, nipo naye.” alisema Mwasipu.

Mbowe, alikamatwa majira ya saa 5 za asubuhi kwenye maeneo ya Magomeni mara baada ya kushuka kwenye gari lake.

“Maandamano ni haki ya kikatiba, pale nguvu kubwa kama hii inavyotumika kukusanya askari wengi, ambao wana silaha na gharama kubwa kwa mlipa kodi wa nchi hii nafikiri si sawa sawa” alisema Mbowe baada ya kuzingirwa.

Kamanda wa polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alizungumza na wanahabari na kukiri kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA na watu wengine 14 kwa kile walichosema kukakaidi tamko la jeshi la polisi, la kuendelea kupanga lakini kutaka kufanya maandamano hayo, ambayo tayari yalizuiwa na jeshi la polisi.

Tizama zaidi:

Polisi Tanzania wamkamata Freeman Mbowe

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kwa mujibu wa Mwasipu, mtoto wa Mbowe, Nicole Freeman Mbowe naye alikamatwa na polisi na kupelekwa makao makuu ya Polisi akiwa pamoja na baba yake.

Tangazo la maandamano ya Chadema lilitolewa na Mwenyekiti Mbowe Septemba 11, 2024, ambapo alisema CHADEMA itaingia barabarani wendapo wanachama wao waliopotea hawatarudishwa na kama serikali haitawajibika ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kwa viongozi husika.

Maandamano haya yaliyoitishwa na CHADEMA yanafuatia mfululizo wa matukio ya watu kutekwa na wengine kuuawa. Kadhalika Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho kanda ya temeke, Deusdedith Soka, naye anadaiwa kutoweka tangu Agosti 18 mwaka huu na mpaka sasa hajulikani alipo.

Related Posts