Songea. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuwakataa wanaotaka kuwagawa kwa sababu za kisiasa au tofauti za kiitikadi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 23, 2024 wakati akifunga Tamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika katika Uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma.
Amewasisitiza Watanzania kuwa ni wamoja, wenye nia moja, hivyo hawana sababu ya kutofautiana.
“Niwaombe Watanzania tuwakatae wanaotaka kutugawa kwa sababu za kisiasa au tofauti za kiitikadi. Watanzania ni wamoja nia yetu ni moja sisi ni mtu mmoja,” amesema.
Sambamba na hilo, ameeleza juu ya uwepo wa changamoto ya mmomonyoko wa maadili, akiitaka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kulikabili hilo.
“Kutokana na mwingiliano wa tamaduni kutoka nje tumeanza kushuhudia mmomonyoko wa maadili na vitendo visivyofanana na Utanzania,” amesema.
Ametaka kila Mtanzania abebe jukumu la kukagua na kurekebisha maadili kwenye boma lake.
Ameitaka wizara kushughulikia changamoto ya mmomonyoko wa maadili, kwa kuweka bayana vitu vinavyopaswa kufanyika ili kupata suluhu.
Katika hotuba yake hiyo, amegusia utamaduni kuwa umefungamanishwa na misingi thabiti ya umoja, mshikamano, upendo na utulivu.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kadri maendeleo yanavyokuwa, yaende sambamba na misingi hiyo ya wazee.
“Naridhika kwamba kazi yangu ya kwanza ninayoifanya hapa Ruvuma ni kufunga tamasha la utamaduni Songea, lililofungamanishwa na tamasha la Majimaji Serebuka,” amesema.
Kuhusu tamasha hilo, Samia amesema limekuwa na ushiriki mkubwa kama ilivyoshuhudiwa.
“Nimeambiwa hapa kuna vikundi zaidi ya 20 vimeshiriki hapa katika tamasha hili. Na nashukuru mmealika na wenzetu kutoka upande wa pili wa muungano,” amesema.
Amewakaribisha mabalozi wa nchi mbalimbali waliojumuika na wahudhuriaji wa tamasha hilo.
Aliifungamanisha hotuba yake na rejea ya moja ya hotuba za Baba wa Taifa, inayoonyesha umuhimu wa tamaduni za asili miaka 60 iliyopita.
Amesema Serikali inafanyia kazi maneno hayo ya Mwalimu Nyerere kwa vitendo na hiyo ni kielelezo cha uhai wa tamaduni.
Amesema fursa za kiuchumi zinafunguka kupitia kazi za sanaa, utamaduni unaohusisha vyakula vya asili.
Amewataka wadau wa sekta ya utalii kuona namna ya kuufanya utamaduni kuwa biashara ili uete manufaa ya kiuchumi.
“Nimefurahishwa nilipopita banda la Basata wanaifanya sanaa kuwa biashara na uchumi. Kwa matamasha ijayo muitumie vema fursa hii kutangaza vema,” amesema.
Ameeleza namna watu walivyohangaika kupata nyumba za kulala, iwe fursa kwa wafanyabiashara kuongeza uwekezaji katika myumba za kulala
Kuhusu ziara yake mkoani humo, Rais Samia amesema atakutana na wazee leo jioni na wananchi, kadhalika miradi ya maendeleo.
Amesema atatumia ziara hiyo kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa kwa fedha za Serikali na kuzindua ile iliyokamilika.
Zaidi ya watu 19,000 wanakwenda Songea kwa wiki kupitia uwanja wa ndege uliopo wilayani humo.
Amesema idadi hiyo ni tofauti na ile ya mwaka juzi ambayo ni watu 3,000 pekee.
Mbali na hilo, amesema Tanzania kwa sasa inalenga kufungua vituo 100 vya Kiswahili duniani kwa kushirikiana na Watanzania waliopo nje.
Amesema Watanzania waliopo nje, wanapaswa kutumia fursa hiyo na vijana wengine wenye ubunifu kwa njia ya mtandao watumie fursa hiyo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, Rais Samia amesema kila mwenye sifa ya kupiga kura ahakikishe anakwenda kupiga kura.
Amesema uchaguzi ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa, hivyo vema kuendelea kudumisha amani, kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro, amesema mzizi wa tamasha hilo ni maelekezo ya Rais Samia aliyoyatoa mwaka 2021 akitaka matamasha hayo yafanyike nchi nzima kwa mikoa mbalimbali.
Amesema kauli mbiu katika tamasha hilo ni, ‘Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza.’
Ndumbaro ameielekeza hotuba yake kwa kufafanua utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo kupitia falsafa ya R4 za Rais Samia.
R hizo ni Maridhiano, Utahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya.
Amesema kinachofanyika ni kuhakikisha kupitia matamasha hayo, makabila yote nchini yanakutanishwa kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali.
Sambamba na kujadiliana, amesema makabila hayo pia yanaonyeshana tamaduni zao na kukubaliana utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla.
“Katika mazungumzo hayo tunakubaliana upi ni utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla,” amesema.
Dk Ndumbaro amesema wizara hiyo inafanya mabadiliko hasa kwenye utamaduni, sanaa na michezo kwa kuhakikisha zinakuwa sekta zitakazozalisha ajira na uchumi.
Amesema sekta hiyo kwa sasa inakuwa kwa kasi kwa asilimia 17, huku wasanii 214 wakinufaika na mfuko wa sanaa kwa kukopeshwa Sh2.4 bilioni.
Kuhusu michezo, amesema mabadiliko yamefanyika kuhakikisha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inakuwa na matokeo mazuri hata katika mechi za ugenini.
Sambamba na hayo, Dk Ndumbaro amemuomba Rais Samia amvumilie kwa miaka miwili kuhakikisha sekta ya sanaa, utamaduni na michezo inachangia asilimia nne katika pato la taifa.
Pia, amesema wanajipanga kuhakikisha katika mashindano ya riadha katika mwaka ujao, Tanzania inarudi na medali.
Awali akiwatambulisha wageni mbalimbali katika tukio hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa amesema walipanga tamasha lifanyike Julai lakini baadaye wakapanga kulifanya Agosti mwaka huu.
“Tamasha halikufanyika kinyonge, wamekuja mawaziri karibu nusu ya Baraza lako la Mawaziri,” amesema Msigwa.
Amesema zaidi ya wakuu wa mikoa 10 wamehudhuria tamasha hilo, jambo alilosema ni ishara ya kufana kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Msigwa, katika tamasha hilo vikundi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi vimeshiriki ikiwemo India.
Akizungumza katika tamasha hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Abbas Ahmed Abbas amesema uwepo wa Hospitali ya Mkoa huo, umewezesha wananchi wa ndani na hata nje ya nchi kupata huduma.
Kwa mujibu wa Kanali Abbas, sambamba na wagonjwa kutoka mkoani humo, hospitali hiyo imewezesha wananchi kutoka mataifa ya Msumbiji na Malawi kwenda kupata huduma.
Kwa kuwa shughuli kuu ya mkoani humo ni kilimo, amesema uwepo wa ruzuku ya mbolea umewawezesha wakulima kumudu gharama za mbolea hiyo ili kukuza kilimo.
“Shughuli kuu ya kiuchumi mkoani Ruvuma ni kilimo na Serikali imewezesha kupata mbolea kwa bei nafuu, baada ya kuweka ruzuku, hii imekuza sekta ya kilimo,” amesema.
Amesema kwa sasa mkoani humo barabara zote zinapitika wakati wote na kwamba changamoto chache zilizobaki mamlaka husika zinashughulikia.
Vijiji 551 vya mkoa huo, amesema vimeunganishiwa umeme na vitongoji vichache ambavyo havijapata vinaendelea kuunganishwa.