Sanamu la Nyerere lililobomolewa Tabora laanza kujengwa upya

Tabora. Siku chache baada ya watu wasiofahamika kuvamia na kuvunja sanamu la Mwalimu Julius Nyerere katika Manispaa ya Tabora, mkuu wa mkoa huo, Paul Chacha amesema Serikali imeanza ujenzi la sanamu hilo ambalo lina historia na mkoa huo kwenye harakati za kusaka uhuru wa nchi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 23, 2024 baada ya kutembelea eneo hilo, Chacha amesema uchunguzi wa awali umebaini watu wenye imani za kishirikina ndio waliovamia na kuvunja sanamu hilo.

“Sanamu la Mwalimu Nyerere lilivunjwa na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia Septemba 21, kwa uchunguzi wa awali unaonyesha watu wenye imani za kishirikina ndio walihusika na uharibifu huo, jitihada za kuwanasa zinaendelea lakini ujenzi wa kuhakikisha alama hiyo muhimu kwenye mkoa wetu unaendelea” amesema na kuongeza;

“Baada ya ukarabati mkubwa kufanyika kwenye mnara huu wa kumbukumbu ya hayati Nyerere, tutahakikisha eneo hili hakuna shughuli yoyote inayofanyika, lakini pia tutahakikisha eneo letu linakuwa na ulinzi ili wahalifu wasilifikie sanamu kama ilivyokuwa awali.”

Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee mkoani Tabora, Harun Mbeyu, ameeleza masikitiko makubwa kutokana na uvunjwaji wa sanamu la kihistoria, akitoa wito kwa vyombo vya usalama kuwatafuta na kuwachukulia hatua waliofanya uharibifu huo.

“Unajua hapa ndipo Mwalimu Nyerere alihutubia wananchi na kutokwa na machozi akidai uhuru kutoka kwa wakoloni. Mkutano huo ulifanyika baada ya kupigwa kura tatu za busara za kumwondoa mkoloni, hivyo eneo hili lina historia kubwa sana ya harakati za ukombozi wetu. Tunaiomba Serikali iwatafute waliohusika na sheria ichukue mkondo wake,” amesema Mbeyu.

Diwani wa Mpera, Haruna Msoga, ambaye pia ni miongoni mwa wazee hao, ameeleza sanamu hilo lenye uzito wa kilo 600 ililetwa kutoka mkoani Arusha mwaka 1988 kwa ajili ya sherehe za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa mkoani Tabora, na iliwekwa eneo hilo kwa msaada wa winchi.

Msoga ameongeza kuwa sanamu hilo lilikuwepo kwenye Ofisi za Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora na kwamba waliotekeleza uharibifu huo walidhani sanamu hilo ina madini au walilenga kujinufaisha kupitia ushirikina, ili kupata uongozi.

Related Posts