Serikali yajitosa matibabu aliyekosa Sh200,000 za upasuaji

Mbeya. Siku moja baada ya Mwananchi kuchapisha habari kuhusu Pascolina Mgala (20), mwenye uvimbe mguuni aliyeteseka kwa miaka tisa akiwa ndani, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, imejitokeza kusaidia matibabu yake.

Pia wadau mbalimbali kupitia makundi ya WhatsApp ndani ya Mkoa wa Songwe, wameguswa na hali ya Pascolina na kuanzisha michango kwa ajili ya kumsaidia.

Mwananchi leo Jumatatu Septemba 23, 242 imefika nyumbani kwa binti huyo anayeishi na bibi yake, Lyness Mwampashi (77) ambaye amesema Serikali imeamua kubeba jukumu la matibabu yake.

Amesema analishukuru Gazeti la Mwananchi, Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kwa jumla kwa kuguswa na ugonjwa wa mjukuu wake.

“Ninafurahi kwa hatua hii, nawashukuru sana. Nawashukuru Watanzania na Rais kwa kuguswa na hili la mjukuu wangu. Leo asubuhi gari limekuja kumchukua wanampeleka kwenye matibabu, ameenda na mama yake mkubwa na mjomba wake,” amesema Lyness, ambaye amebaki peke yake nyumbani.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ester Mahawe alipozungumza na Mwananchi kwa simu, amethibitisha kuwa Pascolina amepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa matibabu.

“Kama itahitajika rufaa ya kwenda hospitali kubwa zaidi, tayari nimezungumza na madaktari wataona namna ya kufanya na sisi kama Serikali tutaendelea kusaidia,” amesema Mahawe.

Hata hivyo, Sikujua Msukwa, mtoa huduma ngazi ya jamii aliyekuwa ameongozana na binti huyo, amesema tayari wameelekezwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa matibabu zaidi.

Diwani wa Nambinzo, Hamis Vundwe amesema; “Rais Samia anasikiliza kilio cha wananchi wake na ndio maana leo hii mtoto huyu amepelekwa kwenye matibabu zaidi, tunamshukuru sana.”

Safari ya maumivu, changamoto za matibabu

Pascolina anasema Aprili 16, 2015, alijikwaa wakati akitoka dukani na kupata jeraha ambalo alidhani ni la kawaida, angepona haraka.

Lakini anasema kadri siku zilivyokuwa zikienda, hali ilibadilika kwa mguu kuvimba tofauti na kipele kilichokuwa kimejitokeza baada ya kujikwaa.

Pamoja na machungu aliyopitia, binti huyu anasema hakukata tamaa ya kwenda shuleni. Alikuwa akisoma Shule ya Msingi Mageuzi darasa la nne wakati ameumia.

Alihitimu elimu ya msingi akiwa na jeraha hilo na alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari Malama ambako safari yake ya elimu ilikatishwa akiwa kidato cha kwanza, baada ya kuzidiwa na ugonjwa.  Kama asingeandamwa na ugonjwa huo, ilikuwa ahitimu mwaka huu 2024.

“Nikawa najikuna kawaida pale palipokuwa na kidonda cha kujikwaa, pakawa panaonekana kama panapona, lakini kadri siku zilivyokuwa zinaenda, nikawa nahisi mabadiliko kwenye mguu wangu, ukawa unavimba, baadaye bibi alinipeleka hospitali hapa kijijini,” anasimulia binti huyo.

Anasema hospitali walipobaini ugonjwa ni mkubwa wakampa rufaa ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ambako alifanyiwa upasuaji na eneo aliloumia walitoa kijiwe.

“Ila baada ya mwezi mmoja kupita, nyuzi za kidonda zilifumuka, kwa kuwa hatukuwa na hela za kwenda kutibiwa tena, nikakaa tu nyumbani nikawa nasaidiwa na bibi na watu wengine, lakini ndiyo mguu ukawa unazidi kuvimba na kidonda nacho kikawa kinaongezeka ukubwa,” anasema Pascolina.

Anasema mwaka 2019, baada ya hali kuwa mbaya zaidi, bibi yake alimpeleka Hospitali Teule ya Ifisi ambayo ipo Mbalizi na baada ya vipimo, alitakiwa afanyiwe upasuaji mwingine na gharama yake waliambiwa ni Sh200,000.

“Ukumbuke muda wote huo nilikuwa naugulia tu maumivu nyumbani, sina msaada wowote,” anasema.

Akizungumza kwa kujiamini, Pascolina anasema amepitia maisha magumu kutokana na ugonjwa huo, hata kufikia kunyanyapaliwa na watu waliotakiwa kuwa karibu naye kumfariji.

Anasema mama yake mzazi ambaye kwa sasa anaishi Chunya, kuna kipindi alitaka kumchukua  akaishi naye, lakini bibi alikataa.

“Aliwaambia watu kuwa ni mwizi wa watoto na alikuja kuniiba, alinusurika kushambuliwa na kundi la watu wa hapa kijijini, basi mama hakunichukua tena akaniacha,” anasema.

Anasema kilichomuokoa mama yake asishambuliwe ni barua aliyoibeba kutoka Chunya.

“Aliwaonyesha kwamba yeye sio mwizi wa watoto, ila ni mama yangu mzazi amekuja kunichukua, ile barua alikabidhi kwa mwenyekiti wa kijiji, mama aliandikiwa na viongozi kutoka Chunya aje aikabidhi kwa mwenyekiti kusudi aruhusiwe kunichukua, wananchi waliposomewa, ndiyo wakaamini wakamuacha na wengine wakawa wanamuambia bibi amuache anichukue, lakini alikataa,” anasema binti huyo.

Related Posts