Ushindi huo unampa Kansela Scholz ahueni dhidi ya ukosoaji unaomkabili kuhusu uongozi wake ndani ya chama hicho.
Chama cha SPD kilipata ushindi wa dakika za mwisho katika jimbo la mashariki mwa Ujerumani la Brandenburg, ambako kimekuwa kikiliongoza tangu kuungana tena kwa Ujerumani mbili mwaka 1990.
Kulingana na shirika la habari la Ujerumani la dpa, matokeo ya awali yanaonesha kuwa, chama hicho cha Kansela Scholz kimepata ushindi wa asilimia 31 dhidi ya asilimia 29 za AfD.
Soma zaidi: Chama cha SPD chaongoza kwa ushindi mwembamba dhidi ya AfD Brandenburg
Akizungumza baada ya matokeo hayo ya awali yaliyotolewa Jumapili jioni, Gavana wa jimbo la Brandenburg Dietmar Woidke ambaye aliapa kujiuzulu ikiwa chama cha AfD kingepata ushindi, alisema kuwa, “Ni ushindi muhimu kwangu, ni ushindi muhimu pia kwa chama changu na kwa jimbo la Brandenburg, kwa sababu madhumuni yetu makubwa mwanzoni mwa kampeni yalikuwa kuhakikisha tunaimarisha jimbo letu na kuwa na utulivu wa kisiasa. Na ninafikiri kwa matokeo haya sasa tuna uwezekano wa kupata serikali imara katika miaka mitano ijayo, na hicho ndicho tulichokitaka tangu mwanzo.”
Wengi washiriki kupiga kura
Katika uchaguzi huo watu karibu milioni 2.1 walijiandikisha kupiga kura kwa ajili ya bunge jipya la jimbo hilo. Hivi karibuni, kura ya maoni katika jimbo la Brandenburg iliashiria kuwa Chama mbadala cha Ujerumani cha AfD kinatoa upinzani mkubwa kwa SPD kinacholiongoza jimbo humo kwa muda mrefu.
Kushindwa kwa SPD katika uchaguzi huo kungeonekana kuwa ishara mbaya kwa Kansela Scholz, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka 2025.
Licha ya ushindi wa chama hicho cha mrengo wa kati kushoto, kina asilimia 15% pekee katika kura ya maoni ya kitaifa ya hivi karibuni wakati AfD kikiwa na karibu asilimia 20%. Vyama vingine vya upinzani vimepata asilimia 32 ya kura hiyo ya maoni.
Soma zaidi:
Wiki iliyopita, Meya wa Munich ambao ni mji wa tatu kwa ukubwa Ujerumani alikuwa mwanachama wa tatu wa SPD kupendekeza kuwa chama hicho kinapaswa kufikiria kumteua Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius kuwa mgombea wa Ukansela katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Hata hivyo watu wa ndani ya chama hicho wanasema Kansela Scholz ambaye ameshatangaza nia ya kutetea kiti chake, hana mpango wa kukaa kando katika uchaguzi huo ujao huku akiungwa mkono na maafisa wa ngazi ya juu wa SPD.