Songea. Kama ungepita nje ya Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma, shangwe zinazosikika ungedhani kuna mchezo wa mpira wa miguu unaendelea.
Nderemo na vifijo vinavyosikika vinaakisi furaha ya wananchi ndani ya uwanja huo, baada ya burudani mbalimbali za muziki na kitamaduni zinazopamba tamasha la tatu la utamaduni nchini.
Isingewezekana kukaa hata sekunde bila kudemka, kwani kila aina ya burudani inayogusa kila rika na jamii inasikika katika uwanja huo, wakati ambao Rais Samia Suluhu Hassan akisubiriwa kuhudhuria, akiwa ndiye mgeni rasmi.
Mbali na burudani za muziki, aina ya mavazi hasa ya jamii za Wangoni yaliyonakshiwa na ngozi ya chui, ni jambo lingine linalovutia katika sherehe hizo.
Ukiachana na vazi hilo la kingoni, khanga, vitenge na vazi la kimasai, ni aina nyingine ya mavazi yaliyosheheni kwa wahudhuriaji yakishonwa kwa mitindo tofauti ya kisasa na kale.
Mbwembwe zote hizo, zinalenga kuonyesha mitoko ya kitamaduni, ili kuakisia uhalisia wa siku husika.
Mpaka saa 4:30 asubuhi, ni mapengo machache yaliyokuwepo kwa ajili ya wananchi kujaza uwanja huo, wenye uwezo wa kuchukua watu takriban 10,000.
Pamoja na kiu ya kujulikana mikoa mitatu itakayoibuka mshindi wa masuala ya utamaduni nchini, shauku nyingine ni kuwashuhudia wanamuziki nguli katika jukwaa, akiwemo Diamond Platnumz.
Nikuibie siri kidogo ya uhalisia wa hali ilivyo katika Mji wa Songea katika siku za tamasha hilo. Ilivyo ngumu kumuona Ngekewa, ndiyo ugumu uliofanana na kupata chumba cha kulala wageni, vyote vimejaa.
Ilikuwa afadhali kwa wewe mgeni upate angalau eneo la kuegesha na kuhifadhia vitu vyako, lakini ukisubiri nyumba ya kulala wageni, subira yako isingezaa matunda.
Hili ni tamasha la tatu la utamaduni kufanyika nchini, la kwanza lilifanyika Mwanza, kisha Njombe na sasa ni Ruvuma, dhamira ni kuimarisha umoja wa kitaifa na kudumisha amani kupitia urithi wa utamaduni wa nchi.
Hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhamasisha uzalendo na kudumisha amani, hasa kwa vijana ambao ni nguzo muhimu katika kujenga Tanzania ya leo na kesho.
Hata hivyo, kufanyika kwa matamasha hayo ni matokeo ya maelekezo ya mkuu huyo wa nchi, Rais Samia alipotaka shughuli hizo zifanyike kila mwaka na mikoa tofauti tofauti.
Kabla ya kilele kinachofanyika leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, siku tatu za tamasha hilo ziliwashangaza wengi hasa kwa ngoma za asili kutoka mikoa ya Mwanza, Dodoma na Tanga.
Ngoma za bugobogobo kutoka Mwanza na zile za unyago kutoka Pwani ziliibua hisia kali miongoni mwa wahudhuriaji, wakionyesha urithi wa Tanzania una nguvu katika kuleta watu pamoja.
Tamasha hilo linahitimishwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), sekta ya sanaa na utamaduni imechangia takriban asilimia tatu ya pato la taifa kwa mwaka 2023.
Hii ni ishara kuwa utamaduni si tu sehemu ya urithi, bali ni chanzo cha ajira kwa maelfu ya vijana.
Takwimu hizo zinaonyesha zaidi ya vijana 100,000 wameajiriwa moja kwa moja kupitia sekta ya sanaa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kutoka mwaka 2020.
Ripoti ya Unesco ya mwaka 2022, imeweka bayana utamaduni na sanaa ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi zaidi Afrika, zikitarajiwa kuongeza pato lake hadi asilimia tano ifikapo mwaka 2025.