Ulinzi waimarishwa Mahakama ya Kisutu, kila anayeingia anakaguliwa

Dar es Salaam. Wakati leo Jumatatu Septemba 23, 2024 hatima ya dhamana ya meya wa zamani wa Ubungo, jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai ikitarajia kutolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ulinzi umeimalishwa kuanzia nje hadi ndani ya viunga vya mahakama.

Mwanachi imeshuhudia ulinzi kuanzia getini kwa wale wanaoingia mahakamani hapo, wapo wanaoruhusiwa na wengine wakizuiwa.

Mbali na kukaguliwa, magari yote yanayoingia nayo yanakakuliwa kabla ya kwenda kuegeshwa maegesho yaliyopo ndani ya Mahakama hiyo.

Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa, aliwahi kuwa meya wa Manispaa ya Ubungo, anakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka mawili, likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao.

Alipandishwa kizimbani katika Mahakama hiyo, Alhamisi ya Septemba 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili, ambayo hata hivyo aliyakana.

Baada ya kusomewa mashtaka yake, upande wa mashtaka uliowasilishwa na jopo la Mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hata hivyo, uliwasilisha maombi mawili, la kwanza Mahakama itoe amri ya vifaa vya kielektroniki vya mshtakiwa (simu pamoja na akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) viweze kuingiliwa kwa ajili ya upelelezi.

Ombi la pili, Mahakama izuie dhamana yake kwa kile ilichoeleza ni kwa ajili ya usalama wa mshtakiwa.

Hata hivyo, maombi hayo yote mawili yalipingwa na jopo la mawakili wa utetezi lililoongozwa na Peter Kibatala, pamoja na mambo mengine walidai yamewasilishwa kinyume na utaratibu wa matakwa ya kisheria na kwamba kiapo kilichotumia kuwasilisha mahakamani maombi hayo kina kasoro za kisheria.

Sambamba na hoja za kupinga maombi hayo ya Serikali, pia mawakili wa utetezi waliiomba Mahakama impe dhamana mshtakiwa huyo, wakidai dhamana ni haki ya kikatiba.

Hoja hizo za mawakili wa utetezi pia zilipingwa vikali na mawakili wa Serikali, Katuga na Wakili wa Serikali, Job Mrema, huku wakisisitiza uhalali na umuhimu wa hoja zao kuhusiana na maombi yao.

Baada ya mvutano mkali wa hoja za kisheria kuhusiana na uhalali wa maombi hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo hadi aliiahirisha hadi leo Septemba 23, 2024 kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Mpaka saa 5:40 asubuhi, keshi ilikuwa haijaanza. Mawakili wa pande zote mbili wameshafika mahakamani.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts