Vibatari vilivyozaa Soko la Makoroboi Mwanza

Mwanza. Ukifika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza ukahitaji kununua nguo hususan ‘mitumba’ eneo utakaloelekezwa na wenyeji ili kujipatia bidhaa hiyo kwa bei rahisi ni ‘Makoroboi’.

Makoroboi ni eneo linalopatikana katikati ya Jiji la Mwanza, likipakana na mlima ilipojengwa nyumba ya Gavana wa mwisho wa Tanzania, Richard Turnbull ambayo sasa imegeuzwa kuwa eneo la kihistoria na linalotumiwa kwa ajili ya kambi ya mafunzo mbalimbali.

Upande wa mashariki, Makoroboi inapakana na Mtaa wa Rwagasore linapojengwa Soko Kuu la Mwanza ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 96 kwa gharama ya zaidi ya Sh23.3 bilioni.

Makoroboi kama ilivyo sifa yake, ni eneo ambalo linatumiwa na wafanyabiashara wadogo maarufu kama ‘Machinga’ ambao husifika kwa kuuza bidhaa ikiwemo nguo  kwa bei rahisi.

Pamoja na kusifika kutokana na kushamiri kwa biashara ya nguo zinazouzwa kwa ‘bei chee’, asili ya neno Makoroboi haitokani na nguo, bali ni vibatari ambavyo vilipachikwa jina la ‘Korobhoi’ ama ‘Koroboi’ na watu wenye asili ya India.

Mwanzilishi wa soko la Makoroboi jijini Mwanza, Mzee Juma Athumani, akizungumza na mwandishi wa makala haya

Mwanzishili wa soko hilo na mtengenezaji wa vibatari  au koroboi’ Juma Athuman (75) anasema soko hilo lilianzishwa zaidi ya miaka 68 iliyopita wakati huo eneo hilo likiitwa Nyamagana.

“Tulianza kutengeneza koroboi katika eneo hili kabla ya kuja machinga katika eneo hili, tulikuwepo watengeneza koroboi peke yetu. Tumekaa hapa ndiyo wakaanza kuja machinga wakati wa awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985,” anasema mzee Athuman.

Mzee Athuman ambaye anatamba kujifunza utengenezaji wa koroboi kutoka kwa babu yake,  Juma Shokoro,  anasema baada ya  uhitaji wa koroboi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuongezeka walianzisha Umoja wa Mafundi Koroboi Nyamagana (UMKN).

Hata hivyo, mabadiliko ya tabianchi hayajaliacha salama jina la Makoroboi kwa kile kinachotajwa na Athuman kuwa ni mabadiliko ya malighafi inayotumika kutengenezea koroboi hizo kubadilika kutoka za chuma hadi sasa kutumika plastiki na aluminiun.

“Tuliendeleza jina la Makoroboi kwa sababu vibatari vilihitajika kwa kiwango kikubwa lakini sasa hivi teknolojia imekua havitumiki maeneo mengi. Hata  hata vibaba vya kupimia mafuta vimebadilika sasa hivi matokeo yake tumeamua kuishi kwa kutengeneza masanduku ya chuma,” anasema.

Anasema eneo hilo litaendelea kuibeba sifa yake pamoja na kuwepo ongezeko la watu na wafanyabiashara,  huku watengenezaji wa vibatari na masanduku hayo wakipungua kutokana na uhitaji wake kupungua.

“Unaweza kuangalia hapo kiwanda kizima kuna koroboi  hazifiki hata 100. Lakini wakati huo ungekuta eneo lote hili zimejaa halafu kuna misururu ya wateja wanasubiria kusafirisha kwenda maeneo mengine kama Burundi na mikoani,” anasema.

Remmy Ongala atembelea Makoroboi

Kwa mujibu wa Athuman, Makoroboi ilipata umaarufu zaidi mwaka 1992 baada ya kutoka kundi la Orchestra Super Matimila chini ya kinara wake, Remmy Ongala kutembelea soko hilo na kufanya tamasha lililoambatana na kuimba na kucheza muziki na wafanyabishara wa eneo hilo.

“Remmy Ongala alikuja hapa kutembea Makoroboi hata kwenye muziki wake aliimba ukija Mwanza usiache kutembelea Makoroboi tukaimba naye pale sasa walipokuja machinga nao wakasema wanafanya biashara eneo la makoroboi,” anasema.

‘Tuligoma kuhamishwa’

Athuman anadai pamoja na jitihada za kuwahamisha machinga katika eneo hilo kwenda katika masoko yaliyojengwa na Serikali ili kuondoa msongamano na kuepusha kufanya biashara maeneo yaliyokatazwa, jitihada hizo ziligonga mwamba kwao kwani wao ndiyo makoroboi.

“Sisi walitaka kutuchanganya na machinga tukasema hapana tukasema sisi ndiyo makoroboi japo walitaka kutuchanganya na machinga. Niliwaambia vijana ‘wanachama’ wa umoja wa watengenezaji koroboi ili kulinda hadhi ya eneo hilo,’’ anaeleza.

Anasema mchakato wa kusajili jina la eneo hilo umeshaanza ili kulinda hadhi na jina hilo ili lisipotee.

“Kati ya watu tisa ambao tulianzisha hili soko miaka zaidi ya 63 iliyopita nimebaki mimi peke yangu hapa. Nimekuwa nikiwashauri vijana wengine waliojiunga kwenye umoja wetu kuendelea kurithisha ujuzi huu wa kutengeneza koroboi kwa wenzao ili kuhakikisha tunalinda asili na jina la Makoroboi kwa kizazi hiki na kijacho,” anaeleza.

Related Posts