Makundi mengine ya haki za binadamu yanasema watu wa jamii hiyo walilazimishwa kujiunga na jeshi la Myanmar hali iliyochochea mashambulizi ya kulipa kisasi kutoka kwa jeshi la ukombozi la wanamgambo wa Arakan.
Katika matukio mabaya yaliyowahi kurekodiwa, Shirika linalofuatilia Haki za Binadamu la Fortify lilisema mwezi uliopita kuwa, waasi wa Arakan waliwauwa zaidi ya wanaume 100 wa Rohingya, wanawake na watoto katika shambulio la droni kwenye eneo la mpaka.
Arakan mara zote wamekanusha kufanya uhalifu
Wanamgambo wa Arakan mara kadhaa wamekanusha kuhusika katika shambulio hilo na madai ya kuwa waliwalenga raia wa jamii hiyo kwa ujumla. Licha ya hilo, maelfu ya wakimbizi wanaokimbilia Bangladesh wanalishutumu kundi hilo kwa kuhusika na uhalifu huo.
Soma pia:Jumuiya ya ASEAN yatoa wito wa kuwepo suluhisho la amani kwa mizozo ya Myanmar, Ukraine na Gaza
Mmoja wa wakimbizi wa jamii ya Rohingya aliyejitambulisha kwa jina la Syed, alikimbia mwezi uliopita kwa mara ya pili kutoka Myanmar, baada ya kulazimishwa kupambana upande wa jeshi lililowahi kuifukuza familia yake kwenye ardhi yao kipindi cha nyuma.
Syed, ni mmoja wa maelfu ya vijana kutoka katika jamii hiyo ya wachache ya Waislamu wanaoonewa wasio na nchi wanaokusanywa kupigana kwenye vita ambavyo hawakuvianzisha. Yeye na vijana wengine waliolazimishwa kujiunga na jeshi walipewa kazi kama vile kubeba mizigo, kuchimba mashimo na kuchota maji kwa ajili ya wanajeshi wa Myanmar wakati wanajeshi hao wakiendelea kupambana na waasi
Alifanikiwa kuwatoroka alipopelekwa kulinda doria katika kijiji kimoja kisha akaelekea Bangladesh. Kijana huyo ni miongoni mwa Warohingya 14,000 waliofanikiwa kuvuka mpaka katika miaezi ya hivi karibuni wakati ambapo mapambano yamezidi kupamba moto. Takwimu hizi ni kulingana na Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa.
Vijana walilazimishwa kujiunga na jeshi kusaidia kwenye vita
Syed anasema kuwa kujumuishwa kwao kwa kulazimishwa kujiunga na jeshi la Myanmar kumesababisha ongezeko la mashambulizi ya kulipa kisasi dhidi ya raia na kuwafanya maelfu kukimbilia Bangladesh, nchi ambayo tayari inawahifadhi karibu Warohingya milioni moja.
Anasimulia kuwa awali alilazimishwa kujiunga na kundi la wanamgambo linaloendesha shughuli zake kwenye kambi za wakimbizi mwezi Juni na kisha alipelekwa kupigana dhidi ya jeshi la ukombozi la Arakan, ambalo ni la waasi wanaopigana vita dhidi ya utawala wa kijeshi wa Myanmar ili kulikomboa eneo lake linalojitawala.
Kijana Mohammad Johar mwenye miaka 22, anasema shemeji yake aliuwawa katika shambulio la droni analodai kuwa lilifanywa na wanamgambo wa Arakan wakati walipokuwa wakiukimbia mji wa mpakani wa Maungdaw mwanzoni mwa mwaka.
Soma pia:UN yasikitishwa na mashambulizi ya anga yanayoendelea Myanmar
Anakumbuka kuwa alishuhudia miili ya watu waliokufa ikiwa imetapakaa kila mahali na hata kando ya mto. Anaongeza kuwa katika eneo hilo, jeshi la Myanmar linashindwa kuwadhibiti wanamgambo wa Arakan na kuwa wengi wa wanaokufa kwenye mapigano hayo ni Waislamu.
Bangladesh imekuwa kwenye mapambano ya miaka mingi ya kufanikisha kuendelea kuihudumia idadi kubwa ya wakimbizi iliyonayo, ambapo wengi wao waliwasili nchini humo baada ya jeshi la Myanmar kufanya mauaji katika vijiji vya jamii ya Rohingya, suala linaloendelea kuchunguzwa na Umoja wa Mataifa.
Wakati Bangladesh ikijikongoja baada ya mapinduzi ya ghafla ya serikali yaliyoanzishwa na wanafunzi dhidi ya serikali mwezi uliopita, Waziri wake wa Masuala ya Kigeni, Touhid Hossain alizungumza mapema mwezi huu kuwa kwa sasa kupokea wakimbizi wengine ni suala lililo nje ya uwezo wa Bangladesh.
Baada ya mashambulizi mabaya kabisa dhidi ya Warohingya 600,000 ambao bado wanaishi Myanmar, wakimbizi wapya wanaoingia nchini humo wanasema kuwa hawana njia nyingine bali bali kuvuka mpaka ili kutafuta mahali salama.