Geita. Washtakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya Sophia Sita, Mkazi wa Kijiji cha Kasala wilayani Chato Mkoa wa Geita, wameachiwa huru baada Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Mwanza kabla kurudishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita ilipokuja leo Septemba 23, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Mwandamizi, Luciana Shaban ameieleza Mahakama kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya usikilizwaji, lakini DPP amewasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Nyamarwa Mashauri, Tibasima Kakuru na Lazaro Philipo ambao walidaiwa kumuua Sophia Mei 17, 2018 kwa mwili wake kutenganishwa na kiwiliwili.
Kutokana na ombi hilo, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Athuman Matuma amewaachia huru washtakiwa hao chini ya kifungu cha 91(1) cha mwenendo wa mashauri ya jinai na kwamba kwa mujibu wa akifungu hicho, kuachiwa kwao hakutazuia upande wa Jamhuri kuwakamata siku za usoni watakapowahitaji.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri uliwasilishwa na Luciana Shaban na Kabula Benjamin, huku upande wa utetezi mawakili walikuwa Doreen Narzis, Erick Lutehanga na Paul Michael.
Akizungumza baada ya kuachiwa, Nyamarwa Mashauri amesema anamshukuru Mungu, kwani amekaa mahabusu kwa miaka sita.
“Nimekaa mahabusu hadi macho yangu sasa hayaoni vizuri, hata ndugu zangu wamefika hapa sijawatambua ila namshukuru Mungu nimeachiwa huru. Sina la kusema namshukuru Mungu,” amesema Mashauri.
Naye Lazaro Philipo, amedai awali alikamatwa kwa kosa la kukutwa na mitego ya kuvua samaki na kukaa mahabusu kwa mwaka mmoja, lakini baadaye akashangaa kupandishwa mahakamani na kuunganishwa na washtakiwa wengine.
“Nilikamatwa kwa kukutwa na mitego ya kuvulia, lakini baadaye nilipandishwa mahakamani nikiambiwa nimeua na kuunganishwa na washtakiwa wengine. Huyo mtu hata sikuwahi kumfahamu. Namshukuru Mungu nimeachiwa huru,” amesema Philipo.