Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matiri Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wakimshangilia Waziri wa Maji Juma Aweso(hayupo pichani)baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi wa maji utakaohudumia wananchi zaidi ya 9,000 wa kata ya Matiri.
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
WAKAZI zaidi ya 9,870 wa vijiji vitatu vya Matiri,Kiyaha na Liwihi kata ya Matiri Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, wamepata matumaini ya kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama kufuatia mradi wa maji uliogharimu Sh.bilioni 1.6 kufikia asilimia 98 ya ujenzi wake.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi ulianza kutekelezwa mwezi Mei 2023 kwa kutumia Mkandarasi mzawa M/S Sivikwa Co Ltd aliyelipwa Sh.947,006,156.67 kwa kazi alizotakiwa kuzifanya.
Sinkala alisema,mradi huo umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi tangu mwezi Machi mwaka huu na ulikuwa muda wa mwisho wa mkataba na kwa sasa upo katika kipindi cha uangalizi wa muda wa mwaka mmoja.
Alisema,kwa upande wa Serikali kupitia Ruwasa imenunua bomba kwa gharama ya Sh.724,660,270.00 hivyo kufanya gharama zote za mradi kufikia Sh.1,671,665,426.67.
Alitaja lengo mradi ni kuboresha huduma ya maji katika mji mdogo wa Matiri na vijiji jirani ambapo kumepunguza adha kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na kwa wananchi wa vijiji hivyo tangu ulipoanza kutoa huduma.
Aidha,mradi umewezesha kupungua kwa magonjwa ya mlipuko na kusaidia wananchi kupata muda mwingi wa kushughulika na kazi nyingine za kiuchumi kwa kuwa maji yanapatikana karibu na makazi yao.
Akiongea na wananchi wa vijiji hivyo Waziri wa maji Juma Aweso, amewahakikishia wananchi wa Matri kuwa,hatokuwa kikwazo kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla juu ya kupata maji safi na salama na salama.
Waziri Aweso,amewapongeza wananchi wa Matiri kupata mradi mzuri uliomaliza kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji na kuwataka kuutunza mradi huo na vyanzo vya maji ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo,amemuagiza Meneja wa Ruwasa Mashaka Sinkala pamoja na mkandarasi kuhakikisha wanamaliza kazi zilizobaki ili wananchi waendelee kupata huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
Aweso,amewaomba wananchi wa kata ya Matiri, kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan afya njema ili aweze kuendelea kuwa na nguvu na afya njema ya kuwatumikia Watanzania ambao wanashauku kubwa ya kupata maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Matiri Amos Mhagama,ameishukuru Serikali kupitia Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao umesaidia kuimarisha ndoa na wananchi kupata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.