* Kikwete kuongoza harambee matibabu yao mwezi ujao
Mwandishi Wetu
RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuongoza harambee ya kuchangia matibabu ya watoto 1,500 wanaougua magonjwa mbalimbali ya moyo ili wapate matibabu kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Naibu Spika wa Bunge, Musa Azzan Zungu, wakati akizungumzia harambee hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 2, Novemba mwaka huu kwenye hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam.
Alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa, wawili wanakuwa na matatizo ya moyo na kwamba hadi sasa watoto 1,500 wameandikishwa kwaajili ya kupata matibabu hayo lakini hawana uwezo.
Naibu Spika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Heart Team Africa Foundation, alisema watoto hao wasipopata matibabu hayo kwa wakati wanaweza kupoteza maisha hivyo aliwaomba watanzania kujitokeza wakati wa harambee hiyo kuwachangia matibabu.
\“Nawaomba watanzania tuungane kumuunga mkono rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuimarisha huduma za mama na mtoto. Serikali yake imekuwa ikichangia asilimia 70 ya gharama ya matibabu kwa watoto wanaozaliwa na mataizo ya moyo kwa hiyo ni wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais wetu,” alisema
Alisema watoto wengi wenye matatizo hayo wanatoka katika familia zisizo na uwezo hivyo aliomba taasisi na mashirika mbalimbali kujitokeza kusaidia juhudi za Rais Samia kuwagharamia matibabu watoto hao ili wakatibiwe (JKCI).
Alisema JKCI kwa kushirikiana na taasisi ya Heart Team Africa Foundation wameandaa harambee hiyo kwa ajili ya kukusanya asilimia 30 ya matibabu ya watoto hao ambayo ni sawa na shilingi milioni nne kwa kila mtoto atakayetibiwa.
“Nawaomba watanzania wote, wafanyabiashara, taasisi binafsi na za umma, vilabu vya michezo, wasanii, mabalozi wa nchi mbalimbali na vyombo vya habari tuunge mkono juhudi hizi za Rais Samia Suluhu Hassan katika harambee hii ya kuokoa maisha ya watoto wetu yenye kauli mbiu ya tia nuru, gusa moyo lete matumaini kwa watoto,” alisema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dk Peter Kisenge alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya kwa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu kwa hospitali zote kubwa nchini pamoja na kusomesha wataalamu bobezi.
Alisema madaktari bingwa wa JKCI wamejiandaa kutoa huduma bora za upasuaji kwa watoto na watu wazima watakaokwenda kupata matibabu ya moyo kwenye taasisi hiyo na kuhakikisha maarifa ambayo wataalamu wa taasisi hiyo wameyapata yanawasaidia watanzania na nchi jirani.
“Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati JKCI imeendelea kuwa ndiyo hosptali kubwa na ya kutegemewa yenye vifaa vya kutosha, yenye madaktari bingwa wa kutosha na ambayo mafanikio ya wanaokuja kupata tiba kwetu ni kubwa sawa sawa na wanaopata matibabu nchi zilizoendelea ndiyo maana madaktari bingwa duniani wanapenda kuja hapa nchini kufanyakazi na JKCI,” alisema
Dk. Kisenge alisema uboreshaji wa huduma za afya nchini umewavutia wagonjwa wa nchi mbalimbali ambao wamekuwa wakija kwenye (JKCI) kupata matibabu ya kibingwa.
“Namshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa maono makubwa aliyonayo kwenye sekta ya afya kwani ameendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya ambapo mabadiliko makubwa sana yametokea kiasi kwamba vifaa vya kisasa ambavyo tulilazimika kuvifuata nje ya nchi sasa vinapatikana kwenye hospitali zetu nchini,” alisema