BAADA ya Yanga kuweka rekodi ya kuwachapa Waethiopia ndani-nje na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe, staa wa kikosi hicho cha Jangwani, Stephane Aziz Ki amefunguka kuwa hawana presha ya hatua inayofuata, huku akifichua siri iliyopo katika mkataba wake.
Aziz Ki ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya kufunga mabao 21, mwanzoni mwa msimu huu aliongeza mkataba ambao unaendelea kumfanya aitumikie Yanga aliyojiunga nayo msimu wa 2022-23 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Kiungo huyo ambaye aliongeza mkataba wa miaka miwili ndani ya Yanga, katika mechi nne za mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao manne na kutoa asisti moja.
Raundi ya awali alifunga mabao mawili kati ya 10 iliyofunga Yanga dhidi ya Vital’O ya Burundi, huku katika mechi mbili za raundi ya kwanza akifunga mabao mawili kati ya 7-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz alisema mipango mizuri ya kuongeza mastaa iliyokuwa nayo Yanga ndio iliyomvutia zaidi kusalia kwani aliamini watafanya vizuri msimu huu.
“Niliamua kubaki kwa kuongeza mkataba Yanga kwa sababu nilijua mipango mizuri ya klabu kuwa, itakwenda kuongeza mastaa wakubwa ambao sasa wameianza safari ya kwenda kutafuta taji la Afrika kibabe zaidi.
“Huwezi kufanikiwa bila kuwa na mastaa wazuri ambao kwa pamoja tukiunganisha uwezo tunazalisha ushindi ndio maana nimebaki ili kuwa miongoni mwa mabingwa,” alisema Aziz.
ANACHOKIONA HATUA YA MAKUNDI
Aziz Ki amebainisha kwamba wala hawana presha ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa wana timu imara na benchi bora la ufundi hivyo anaamini kwa ubora wa kikosi walichonacho wana nafasi ya kwenda kufanya makubwa Afrika.
“Tuna kikosi kizuri ambacho kinajua kutengeneza mpango ambayo inanipa urahisi mimi na wenzangu kufunga.
“Endapo ratiba itakayotoka mwezi ujao itatupa urahisi basi tutashtua kwa kufanya makubwa kwani uongozi wetu na hata sisi tunalitaka kombe hilo kubwa Afrika ngazi ya klabu,” alisema.