FCC yatakiwa kujipanga na soko huru la Afrika

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi John Simbachawene ameitaka Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza udhibiti wa bidhaa bandia ili kuwalinda walaji hasa wakati huu ambao soko huru la biashara Afrika linaanzishwa.

Pia, ameitaka kutoa elimu kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili waelewe kuhusu masuala ya bidhaa bandia na jinsi ya kuzidhibiti.

Simbachawene  amesema hayo leo Septemba 24, 2024 baada ya kutembelea ofisi za FCC ili kujifunza shughuli zinazofanywa na tume hiyo.

Dk Simbachawene amesema maofisa hao wakiongezwa kwenye vituo maalumu vya kuingizia bidhaa vilivyopo kwenye mikoa minane vikiwamo vya Bandari ya Dar es Salaam, Tunduma, Holili, Tarakea na Namanga itasaidia kudhibiti bidhaa bandia kuingia nchini.

“Soko huru la biashara Afrika litakapokamilika litakuwa limefungua bidhaa kutoka nchi zote kuingia nchini, hivyo FCC itakuwa na kazi kubwa kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zisiwe za bandia.

“Tulikuwa tunajua bidhaa zinazoingia nchini zinapitia katika Bandari ya Dar es Salaam, lakini kwa kuwa biashara tunayotaka kwenda nayo ni ya soko huria itatulazimu kama nchi kuongeza udhibiti wa bidhaa ambazo hazipo katika viwango,” amesema Dk Simbachawene.

Amesema FCC ikiongeza nguvu katika kutekeleza majukumu yake ili kudhibiti bidhaa bandia, itawalinda walaji pamoja na kuulinda uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya FCC, William Erio amesema Serikali imepitisha sheria itakayowaletea ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zao za kukuza uchumi wa nchi kupitia biashara

“Tunaishukuru Serikali kupitia Bunge kwa kupitisha marekebisho ya sheria ya FCC, sheria iliyopo sasa ilianza kutumika mwaka 2003 na kufanyiwa marekebisho madogo mwaka 2019/ 2020 na mwaka 2021,” amesema Urio.

Related Posts