Hii ndiyo simulizi ya Kimara na mitaa yake

Dar es Salaam. Tofauti na ilivyo katika maeneo mengi, karibu kila jina la mtaa unaounda Kata ya Kimara ni simulizi yenye historia maridhawa.

Uwepo wa viwanda, shughuli za kiuchumi na miradi mbalimbali, ndiyo msingi wa ubatizo wa majina hayo, yanayoendelea kutumika hadi sasa.

Unapotokea mjini , Mtaa wa Kibo ndilo lango la kuingia Kimara. Ingawa Kibo inahusishwa na Kata ya Ubungo, kwa sehemu fulani imeigusa Kimara.

Mwonekano wa eneo la Kimara Temboni. Picha na Michael Matemanga

Historia ya jina Kibo inahusishwa na kilele cha Kibo kilichopo  Mlima  Kilimanjaro kama inavyosimuliwa na Meya mstaafu wa Ubungo, Boniface Jacob kupitia mtandao wake wa X.

Mzee Naumu ndiye mwasisi wa jina hilo, aliyeamua kuipa jina baa yake aliyoijenga katika eneo hilo, Kibo Bar na umaarufu wake ukazaa jina la mtaa hadi sasa panaitwa Kibo kwa mujibu wa Jacob.

Kwa mujibu wa Jacob maarufu Boni Yai, Mzee Naumu aliamua kuiita baa yake kwa jina hilo,  kwa kuwa eneo hilo lilikuwa na mlima na hivyo aliufananisha na kilele cha Kibo.

Kabla ya jina hilo, Jacob anasema eneo hilo liliitwa kilima cha kwanza kwa anayetoka mjini  na kilima cha mwisho kwa anayetokea Mbezi. Hivyo hakukuwa na jina rasmi.

Kwa bahati nzuri Kibo Bar ipo hadi sasa, lakini si kwa umaarufu kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo ni vigumu kuiona unapopita barabarani kwa kuwa mbele yake kuna fremu za maduka na mti ambao ni kijiwe cha madalali.

Ukijiuliza ya Kibo, ya Kimara Baruti nayo yanavutia kutaka kujua. Asili ya jina hilo ni shughuli za uhifadhi baruti zilizokuwa zinafanywa katika eneo la kiwanda cha Saruji cha Twiga Chemical.

Baruti hizo, zilitumika kupasulia mawe yanayotumika katika kutengenezea saruji.

Katika eneo hilo pia, Jacob anasema kulikuwa na maghala ya kuhifadhi baruti na kambi kubwa ya wafanyakazi wa kiwanda cha saruji.

Haikuwawia vigumu Waswahili, kushabihisha shughuli maarufu katika eneo hilo na jina la mtaa na ndilo chimbuko la Kimara Baruti.

Mwanasiasa huyo anasema kwa sasa eneo hilo imejengwa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo na shughuli za uhifadhi baruti zilihamishwa tangu miaka ya 1990.

Kama lilivyo jina lake, asili ya jina la mtaa huu ni bucha la nyama ya kitimoto, lililojengwa kwa nakshi za aina yake kulingana na nyakati hizo, inadaiwa miaka ya 1980, kwa mujibu wa Jacob.

Bucha hilo lililokuwa mali ya Thomas Lyimo ambaye pia alimiliki kiwanda cha maziwa cha Thom Dairy, yaliyokuwa yakigawiwa bure katika shule za msingi.

Alianza kwa kujenga banda la chuma tupu, kwa namna lilivyopambwa kila mmoja alikuwa na shauku ya kujua nini kinalengwa kuwekwa ndani yake.

Hatimaye likawa duka la nyama ya nguruwe na ndiyo asili ya jina la Kimara Bucha.

Hili sio la muda mrefu kama yalivyo majina mengine. Liliibuka mwanzoni mwa miaka ya 1990 kama inavyosimuliwa na Jacob kupitia mtandao huo.

Kabla ya Korogwe, eneo hilo liliitwa Kimara Resort kutokana na uwepo wa kiwanja cha starehe, mithili ya vile  viwanja maarufu hapa mjini kwa sasa.

Watu wa nyakati hizo, kabla ya kwenda kwenye kumbi hiyo, walivalia suti ya kitambaa cha Asante Urafiki, lililokuwa vazi maarufu kipindi hicho.

Mbwembwe na umaarufu wa jina hilo, ulivurugwa na Msambaa aliyetoka Korogwe mkoani Tanga na kuanzia banda la chipsi, msosi pendwa kwa mabinti.

Haikuwa kawaida, kwa kuwa banda hilo lilipanga magari ya Serikali na msururu wa wananchi wakisubiri chipsi za msambaa, pengine kwa sababu ya ladha yake.

Hakuwa peke yake, kama ulivyo utamaduni wa wasambaa, alikuwa na vijana zaidi ya 100 wanaotumikia ofisi hiyo kwa kumenya viazi kukidhi mahitaji ya wateja.

Kwa mujibu wa simulizi ya Jacob, isingekuwa rahisi upite eneo hilo na una fedha mfukoni, usinunue chipi kwa namna zilivyonukia na kuvutia.

Basi bwana, jamaa akapata wazo  akaandika bango kwa mkono ‘KOROGWE’ Kuanzia hapo jina la Resort likajifia na Korogwe likaibuka.

Related Posts