Ishu ya Mpanzu kucheza Simba ipo hivi!

KAMA ambavyo Mwanaspoti lilikujuza mwanzo mwisho dili la winga mpya wa Simba, Ellie Mpanzu tangu anatoka DR Congo hadi anatua Bongo na kusaini mkataba wa miaka miwili, basi kaa kwa kutulia ufahamu kinachoendelea kwa staa huyo lini ataanza kuonekana rasmi uwanjani.

Kumekuwa na mijadala mbalimbali katika vijiwe vya kahawa na mitandaoni huku kila mmoja akisema lake kuhusu Mpanzu kuruhusiwa kuanza kuichezea Simba.

Katika mijadala hiyo, upande mmoja unadai Mpanzu ataanza kuonekana Simba mara tu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakapoanza Oktoba mwaka huu, wengine wakidai haiwezi kuwa haraka hivyo.

Ukweli ni kwamba, Simba tayari imemalizana na Mpanzu lakini ishu iliyobakia ni kuingizwa kwenye mfumo wa usajili ili kuanza kazi rasmi.

Mpanzu aliyesajiliwa na Simba kutoka AS Vita ya DR Congo, anaweza akaanza kucheza Desemba 16 mwaka huu baada ya usajili wa dirisha dogo hapa nchini kufunguliwa Desemba 15.

Ili apate kibali cha kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ikiwa imetinga hatua ya makundi baada ya kuiondosha Al Ahli Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 3-1, lazima Mpanzu awe na leseni ya kucheza Ligi Kuu Bara kama ambavyo kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinavyotaka.

Wikiendi iliyopita wakati Simba inacheza dhidi ya Al Ahli Tripoli, Mpanzu alikuwa jukwaani na baada ya mechi kumalizika, mashabiki walilizonga gari la Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambalo alipanda mchezaji huyo.

Ilichukua takribani dakika nne mashabiki wakiwa wamelizonga gari hilo wakimtaka winga huyo apande juu yake ili awapungie mkono, lakini jambo hilo lilishindikana badala yake gari likaondoshwa.

Simba ilipanga kumtambulisha mchezaji huyo kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lakini haikuwa hivyo kutokana na gari lililombeba mchezaji huyo lilichelewa kufika uwanjani.

Try Again alipoulizwa juu ya utambulisho wa Mpanzu, amejibu: “Kazi ya kutambulisha wachezaji ni ya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally.”

Kwa upande wake, Ahmed amesema: “Dili la Mpanzu limefikia asilimia 80 kukamilika, hivyo tutakapokuwa tayari tutawajulisha.”

Related Posts