Mamlaka za ajira zatakiwa kuwatendea haki watumishi

Dodoma. Naibu Waziri (Ofisi ya Rais), Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amezitaka mamlaka za ajira kuzingatia weledi wakati wa kusikiliza malalamiko ya watumishi ili kuiepushia Serikali gharama pindi malalamiko hayo yanapopelekwa kwenye rufaa.

Ametaja miongoni mwa udhaifu wa mamlaka hizo ni kutotoa fursa ya mtumishi kujitetea anapokuwa ametuhumiwa na matokeo yake ni kuhukumiwa bila kusikilizwa, jambo ambalo ni kinyume cha misingi ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Sangu ametoa kauli hiyo leo  Septemba 24, 2024 mkoani Dodoma  baada ya kushuhudia usikilizaji wa rufaa na malalamiko ya baadhi ya watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliofanywa  na  mamlaka zao za nidhamu katika maeneo yao ya kazi, huku wakitoa utetezi wao mbele ya makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Amesema kamati za uchunguzi zinazoundwa zinapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taarifa zao kama makosa yamethibitika au kutokuthibitika.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiiumiza Serikali kwa kuanza kulazimika kulipa mshahara mtumishi katika kipindi chote alichokuwa amefukuzwa kazi au kusimamishwa.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Hamisa Kalombola amesema mamlaka za nidhamu na ajira zinahitaji mafunzo kwa kuwa, mashtaka mengi yanayoletwa yamejikita kumkandamiza mtuhumiwa bila kujali kuwa naye ana haki zake.

“Tunapokea rufaa na malalamiko mengi kutoka kwa watumishi, watuhumiwa ambao hawajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na mamlaka za nidhamu na ajira na tumekuwa tukitoa uamuzi bila upendeleo wowote kwa sababu tupo hapa kwa ajili ya kusimamia misingi ya haki,” amesema Kalombola.

Related Posts