KOCHA Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin amesema anafurahishwa na mwenendo wa kikosi hicho, lakini jambo analolifanyia kazi kubwa kwa sasa ni kutengeneza balansi nzuri kwenye eneo la kujilinda na kushambulia kwani bado halijamridhisha.
Kauli ya Moallin imejiri baada kikosi hicho kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni juzi ikiwa ni sare ya pili kwenye mechi tano.
“Ligi imeanza kwa ushindani mkubwa na kila timu imejipanga vizuri, malengo yetu yalikuwa ni kushinda ingawa tunashuruku kupata pointi moja kwa sababu ukiangalia haikuwa rahisi, tulizuia vizuri japo tulifanya pia makosa binafsi,” alisema.
Moallin aliongeza kuwa licha ya kutoruhusu bao katika mchezo na JKT, ila upungufu huo ulijitokeza kwenye mechi na Azam FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam Septemba 19, ambapo timu hiyo ilichapwa mabao 4-0.
“Tulikosa utulivu mkubwa wa kujilinda kwa maana ya hakukuwa na maelewano mazuri baina ya mchezaji na mchezaji ndio maana makosa yetu yalikuwa mengi, japo kuna maendeleo mazuri ambayo tunazidi kuyafanyia kazi siku baada ya siku kikosini.”
Katika michezo mitano iliyocheza timu hiyo hadi sasa imeshinda mmoja, sare miwili na kupoteza miwili ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba, ikiwa katika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi tano.