Simba, Yanga bado dakika 270

MUDA wa kuendelea kufanya shangwe la kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, umekwisha na sasa wakongwe wa soka la Tanzania, Yanga na Simba wana kibarua kigumu cha dakika 270 sawa na mechi tatu.

Kibarua walichonacho wakongwe hao kila mmoja ni katika kuwania pointi tisa zinazopatikana katika mechi tatu zijazo za Ligi Kuu Bara kabla ya kufika Oktoba 19 mwaka huu ambapo watakutana wenyewe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Simba wakiwa wenyeji.

New Content Item (1)

Yanga iliyojikatia tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa pili mfululizo, mechi zao tatu zijazo za ligi itacheza ndani ya siku tisa kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 3. Kisha itapata mapumziko ya siku 16 kujiandaa kuikabili Simba.

Kwa upande wa Simba, nayo itakuwa na muda kama huo wa kucheza mechi tatu mfululizo kuanzia Septemba 26 hadi Oktoba 4 mwaka huu. Kisha itakuwa na siku 15 za kujiandaa kuikabili Yanga.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga kesho Jumatano watakuwa ugenini kucheza dhidi ya KenGold kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, mchezo huo utapigwa kuanzia saa 10:15 jioni.

Yanga inakwenda kucheza dhidi ya KenGold ambayo imepanda daraja msimu huu ikiwa haina matokeo mazuri baada ya kupoteza mechi zote tatu ikiruhusu mabao manane na kufunga mawili. Inaburuza mkia katika msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi nne.

Baada ya hapo, fasta Yanga italazimika kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya kucheza mechi ya nyumbani dhidi ya KMC itakayopigwa Septemba 29 kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 3:00 usiku.

KMC nayo haijaanza vizuri msimu huu kwani katika mechi tano ilizocheza imekusanya pointi tano ikishinda mechi moja, sare mbili na kupoteza mbili.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Oktoba 3 Yanga tena itakuwa nyumbani uwanjani hapo kuikaribisha Pamba Jiji mechi ikitarajiwa kuanza saa 12:30 jioni.

Pamba Jiji ikiwa imepanda daraja msimu huu kama ilivyo kwa KenGold, yenyewe mechi tano ilizocheza haijashinda hata moja, lakini imekusanya pointi nne kutokana na sare nne ilizonazo na ikipoteza moja.

Kwa upande wa Simba, itaanzia ugenini keshokutwa Alhamisi kukabiliana na Azam FC kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar saa 2:30 usiku. Ikumbukwe kwamba Azam imeanza kuamka baada ya kuanza ligi kwa suluhu mbili mfululizo kabla ya kushinda mbili zilizofuatia dhidi ya KMC (4-0) na Coastal Union (1-0).

Ikitoka Zanzibar, Simba itakwenda Dodoma kucheza dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri saa 12:30 jioni, hiyo itakuwa Septemba 29. Dodoma Jiji inayonolewa na Mecky Maxime, katika mechi tano ilizocheza imeshinda moja, sare tatu na kupoteza moja.

Oktoba 4, Simba itamalizana na Coastal Union nyumbani kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam saa 10:15 jioni.

Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema: “Baada ya kumaliza majukumu ya kimataifa, tuna ratiba ngumu ya ligi, hivyo hakuna muda wa kupumzika lazima tujiandae kuhakikisha tunauendeleza mwanzo mzuri wetu.”

Naye kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amezungumzia mechi tatu zijazo za ligi akisema hawana namna lazima wazicheze vizuri kujiweka sehemu nzuri katika msimamo.

Yanga ikiwa imecheza mechi moja ya ligi wakati hivi sasa ni raundi ya tano, imeanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar ugenini, wakati Simba ikishuka dimbani mara mbili zote nyumbani ikizifunga Tabora United (3-0) na Fountain Gate (4-0).

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Katika Dabi za Kariakoo tatu mfululizo zilizopita katika michuano tofauti, Yanga imeshinda zote ikiifunga Simba 5-1 katila Ligi Kuu Novemba 5, 2023 kisha ikaiclaza tena 2-1 katika marudiano ya Ligi Kuu msimu uliopita iliyopicgwa Aprili 20, 2024 kabla ya timu hiyo ya Wananchi kuwatambia tena Wekundu wa Msimbazi kwa bao 1-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 08, 2024.

Katika Dabi ya Kariakoo iliyopita, mashabiki wa Simba waliwapigia makofi nyota wao kuwapongeza kwa kiwango cha juu walichoonyesha na ushindani licha ya kuwa timu yao ilikuwa imetoka kupoteza mechi ya tatu mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi.

Jambo hilo lilitokana na Simba kuwa na kikosi kipya, baada ya kusajili wachezaji wapya 15 huku wakiwafungulia mlango wa kutokea nyota wake wengi.

   Kwa kutambua kuwa ilikuwa imekutana na timu imara ya Yanga iliyojaza magalactico wa soka la Bongo, Simba ilicheza vyema licha ya kuwa na muda mfupi tu tangu nyota wake wengi waanze kucheza pamoja tangu waliposajiliwa wakitokea nchi mbalimbali.

Na baada ya kuonyesha kiwango bora juzi wakati wakiing’oa Al Ahli Tripoli ya Libya na kutinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya sita katika miaka saba, Simba inatarajiwa kucheza vyema zaidi ya mechi iliyopita itakapokutana tena na Yanga ambayo nayo imetoka kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 17-0 katika mechi nne za mchujo.

Related Posts