TEMESA kushirikiana na sekta binafsi uendeshaji wa karakana, vivuko

 

WAKALA wa Ufundi na Umeme wa Tanzania (TEMESA) imepanga kuendesha vivuko, karakana na mitambo ya kukodishwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi, ubunifu, ujuzi na teknolojia mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya taasisi za umma kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi umeibuka kuwa njia sahihi na muhimu inayosaidia uanzishaji au utekelekezaji wa miradi ya taasisi za umma.

“Kwa siku za hivi karibuni, idadi ya taasisi za Umma zinanzovutiwa kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa njia ya ubia kati ya setka ya umma na binafsi, imekuwa ikiongezeka jinsi muda unavyozidi kwenda,” Kafulila amesema na kuongeza kuwa sasa ni zamu ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Wakala huo umetangaza fursa adhimu kwa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuonyesha nia ya kuwekeza, kuboresha na kuendesha karakana zake kupitia njia ya Ubia.

Kama invyofahamika na kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha wakala huu, TEMESA ina jukumu la kufanya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali katika karakana ambazo zipo kila mkoa.

Vile vile, inafanya shughuli za uendeshaji wa vivuko vya Serikali na kukodisha mitambo kwa wadau wanaofanya shughuli za ujenzi wa miundombinu.

TEMESA inasimamia mtandao wa karakana 30 katika mikoa 26 nchini, ambazo kwa wastani zinahudumia magari takriban 29,263 kwa mwaka.

Pia, TEMESA inakarabati na kuhudumia magari ya serikali yapatayo 9,183, pikipiki 12,778 na vifaa au mitambo 433. Aidha, TEMESA inaendesha vivuko 32 katika mikoa 12 na maeneo ya kuvuka 22 kote nchini.

Takriban abiria 79,863 na magari 3,696 hupita katika vivuko hivi kila siku. Serikali inajenga vivuko vipya nane ambapo vitano vitafanya kazi katika Ziwa Victoria na vitatu katika Bahari ya Hindi.

“Fursa nyingine za uwekezaji zilizopo kwenye vivuko hivi ni pamoja na ardhi, majengo na miundombinu muhimu kama sehemu za kusubiria abiria, migahawa, ofisi na mifumo mbalimbali,” amesema Kafulila.

Pia, Wakala unamiliki mitambo ya aina mbalimbali 41 kwa ajili ya kukodisha kwa wateja kwenye sekta za umma na binafsi.

Katika nia za kuimarisha ufanisi na ubora, TEMESA imedhamiria kuendesha karakana zake kumi na tatu (13) kwa njia ya ubia. Karakana hizi ziko katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Shinyanga, Kagera, Singida, Iringa, na Mara. Nyingine zipo katika mikoa ya Manyara, Pwani, Lindi, Ruvuma, Njombe, na Simiyu.

Vile vile, wakala unakusudia kuendesha huduma zote za vivuko nchini kupitia kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Mwekezaji ataruhusiwa kukodisha huduma za kivuko chote, kuunda kampuni ya ubia na TEMESA, au kuendesha vivuko vyake sambamba na vivuko vya TEMESA.

Aidha, wakala unakusudia kumshirikisha mwekezaji binafsi katika kutoa huduma za ukodishaji wa vifaa kwa njia ya ubia kati ya TEMESA na mwekezaji.

Hatua hii ya kimapinduzi ya TEMESA inaungwa mkono kikamilifu na mfumo wa kisheria wa utekelezaji wa miradi kwa njia ya ubia, ambapo Kanuni za 36 (b) & (d) za Kanuni za Ubia kati ya sekta ya umma na binafsi za mwaka 2020 kama zilivyorekebishwa mwaka 2023, zinairuhusu TEMESA kuwaalika wawekezaji katika utekelezaji wa miradi yake kwa njia ya ubia.

“Mpango wa TEMESA wa kuboresha karakana zake, vivuko na kutoa huduma ya ukodishaji mitambo kwa njia ya Ubia unatoa matumaini ya kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hizi yaliyopo kwenye soko,” amesema.

Ushirikishwaji wa wawekezaji utaleta manufaa mengi ikiwepo kuvutia teknolojia za kisasa, kuchochea ufanisi wa uendeshaji wa karakana na vivuko pamoja na kuboresha ubora wa huduma za Wakala kwa ujumla wake.

Kituo cha Ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, chini ya uongozi mahiri wa Mkurugenzi Mtendaji wake, David Kafulila, kimekuwa ni kiungo muhimu katika kusaidia taasisi za Umma kubuni miradi inayofaa kutekelezwa kwa njia ya ubia.

Tangu Kituo cha Ubia kilipoanzishwa rasmi mapema mwaka huu, nchi imeshuhudia mabadiliko makubwa kwenye uratibu wa miradi kwa njia ya Ubia.

“Mageuzi makubwa yatazidi kutokea katika miradi ya ubia baada tu ya Kituo kufikia adhma yake ya kutoa huduma zote za ubia ndani ya Kituo (one-stop centre),” amesema Kafulila.

About The Author

Related Posts