KAIMU kocha mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro amefanya kikao kizito na wachezaji ili kubadili mwenendo mbovu wa timu kabla ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania itakayopigwa kesho, Jumatano.
Uamuzi huo wa Lazaro umekuja baada ya kuishuhudia Coastal Union ikipoteza mechi tatu mfululizo, huku ikiwa na pointi moja katika michezo minne ya mwanzo wa ligi.
Lazaro amewaambia wachezaji wake kuwa huu ni wakati wa kuonyesha ukomavu uwanjani na kuacha kufanya makosa yaliyowagharimu kwenye mechi zilizopita.
“Tumekuwa na michezo mfululizo, lakini tunatakiwa kuonyesha utofauti na kupambana ili kuwa katika mwelekeo mzuri,” alisema Lazaro.
Pia aliongeza kuwa wamefanya kazi ya kurekebisha upungufu na kwamba anatarajia kuona mabadiliko katika mchezo huo.
Kocha huyo alieleza kuwa ingawa timu yake imeanza msimu vibaya, lakini anaamini bado wana nafasi ya kurejea kwenye mwelekeo mzuri na kupambania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
“Bado tunauhitaji wa kuendelea kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Lazaro akionyesha dhamira ya kuimarisha timu ili kushiriki tena mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Coastal Union ilishinda kwa bao la Maabad Maulid Maabad, ushindi ambao Lazaro anatumaini utarejeshwa leo ili kuvunja mwendelezo wa vipigo.
Kwa upande wa kocha wa JKT Tanzania, Ahmady Ally alisema kuwa timu yake imejiandaa vizuri kwa mchezo huo na wanatarajia kufanya vizuri.
“Tunajua ubora wa wapinzani wetu. Kwa hiyo tupo tayari kukabiliana nao,” alisema Ally, akionyesha imani kwa kikosi chake ambacho kimetoa sare mfululizo.
JKT Tanzania imetoka sare katika michezo mitatu mfululizo, jambo linaloifanya kuwa na kiu ya ushindi wa kwanza kwenye ligi msimu huu.
Kwa upande mwingine, Coastal Union imekumbana na vipigo vitatu mfululizo, hivyo kila timu inatarajia kuvunja mwiko wa matokeo yasiyoridhisha katika mchezo huo.
Mchezo huu utakuwa na umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili, ambapo ushindi kwa yeyote kati yao utarejesha morali na kuleta matumaini mapya ya kuendelea kupambania nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.