Dar es Salaam. Wataalamu wa masuala ya usalama na amani katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamesema wana imani na Jeshi la Polisi nchini, huku wakikisitiza lisimamie majukumu yake ya kulinda raia na mali zao.
Mbali na msisitizo huo, wamelitaka jeshi hilo kuhakikisha linafanya upelelezi wa kina utakaowezesha kukamatwa waliohusika katika matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea kuripotiwa nchini.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kuripotiwa kuwapo kwa matukio hayo, likiwemo la hivi karibuni la aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao aliyetekwa akiwa ndani ya basi eneo la Kibo Complex, Tegeta, Dar es Salaam, Septemba 6, 2024 na siku moja baadaye mwili kuokotwa Ununio.
Wametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 24, 2024 katika mahojiano wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa masuala ya usalama, amani na ulinzi, katika ukanda wa SADC utakaozungumzia migogoro, hali ya siasa na utawala bora na kupendekeza masuala muhimu kwa Tanzania kuzingatia katika uongozi wake wa asasi ya Troika ya SADC.
Agosti 17, 2024, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya siasa, ulinzi na usalama wa SADC.
Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Sera za Kimataifa Afrika (CIP-Africa), Balozi Omary Mjenga amesema wana imani na Jeshi la Polisi na mpaka sasa bado hawajajua nani amefanya matukio hayo, hivyo wana uhakika jeshi halitalala mpaka lifahamu wahusika.
“Jeshi la Polisi watuhakikishie katika kufanya upelelezi na kukamatwa wote wanaohusika, kwa sababu hatuwezi kuruhusu kundi la watu wachache kuharibu sifa ya Tanzania,” amesema Balozi Mjenga.
Mwanadiplomasia huyo amesema Tanzania ilivyowekwa kijiografia ni pakubwa, kiasi cha nchi kama Burundi na Rwanda kuikimbilia walipokuwa na matatizo.
“Ukiangalia DRC wanakimbilia Tanzania, Uganda vita ya Iddi Amini, mpaka leo tuna sifa nzuri sana, Comoro mnajua tulichokifanya kwenye ile nchi, tuendelee kubaki na sifa hiyo tusiruhusu wachache waharibu amani iliyopo,” amesema.
Akieleza uzoefu wake, Balozi Liberata Mulamula amesema nchi haipaswi kwenda huko, kwani amani ikishapotea ni kazi kubwa kuirejesha.
Balozi Mulamula aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, ametoa wito kwa kila Mtanzania, vyombo vya dola visimamie amani kabla haijatoweka na kwamba matukio hayo yaiamshe Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Tusibweteke, wawe wanasiasa, vyama vya siasa, vyombo vya dola, tusimamie amani yetu tusiiache ikaondoka, ikiondoka tutakuwa katika hali ngumu. Nasisitiza na vyombo vya habari chocheeni amani ndiyo iwe kauli yetu wote,” amesema.
Suala hilo limeungwa mkono na aliyekuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Dk Salim Ahmed Salim (zamani Diplomasia), Balozi mstaafu Dk Mohamed Maundi aliyesema kila nchi ina matatizo na changamoto zake, kwa hiyo vitu vyote vinavyojitokeza ndani ya nchi iwe kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi inahitaji mtazamo wa kwanza kuvishughulikia.
“Ni vema kushughulikia matatizo yanayojitokeza katika nchi yako, mafanikio yanaanza na wewe kwa maana utashindwa hata kumsaidia jirani, lazima uchukue hatua ya kushughulika na matatizo ya ndani. Nchi itakapokuwa salama ndiyo kwa umoja tunaweza kujitoa tukashughulika na matatizo ya nje,” amesema Balozi Maundi.
‘Tanzania siyo kisiwa’
Aliyekuwa Luteni Jenerali Mstaafu, Balozi Paul Mella amesema kuna haja ya kujua Tanzania si kisiwa, yanayotokea pia yanatokea sehemu nyingine, hivyo nchi ina haja ya kujifunza kutoka kwa wengine yalipotokea walichukua juhudi gani kuyadhibiti.
“Ninafahamu imeundwa tume ya kuchunguza hili tukio la mwenzetu mmoja Ali Kibao aliyetolewa kwenye gari na kukutwa amekufa, tukio hili baya sana na mengine. Nadhani taarifa ya uchunguzi itakapotoka, itatusaidia kufanya tathmini nani anayesababisha hayo na nini kifanyike,” amesema.
Awali akifungua mkutano huo wa ndani, Balozi Mjenga amesema mkutano huo unajadili hali ya usalama na amani katika ukanda wa SADC uliokusanya wataalamu kutoka Tanzania, Afrika Kusini, DRC, Msumbiji na Burundi.
Amesema ajenda kubwa ni hali ya usalama na amani katika Kanda ya SADC na ni masuala gani wanaweza kuyapendekeza kwa mwenyekiti ayachukue na kuyaendeleza.
“Tuna matatizo mengi katika ukanda huu, kule Kivu DRC tuna shida, pia Msumbiji Kaskazini tuna matatizo ya ugaidi na sisi tunahusika katika kuleta uelewa. Mkutano huu umeleta wataalamu wa masuala ya usalama, amani na ulinzi wapo waliowahi kuwa wakuu wa ulinzi na usalama, watafiti kutoka UDSM, wataalamu kutoka Namibia na mabalozi wanaohusika na masuala ya Sadc kwenye nchi zao,” amesema Balozi Mjenga.
Amesema wataalamu pia watajadili hali ya siasa na utawala bora katika ukanda wa SADC na kutoa maoni yao kuhusu nini kifanyike, ili kuleta hali ya utulivu katika ukanda. Pia hali ya uchumi wa dunia na ule wa ukanda wa SADC.