Adaiwa kumuua mama yake akigombea mali za marehemu baba yake

Moshi. Adela Mushi (74), mkazi wa Okaseni, kata ya Uru kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro anadaiwa kuuawa kwa kunyongwa na kisha kukatwa na shoka sehemu ya usoni na mwanaye, anayedai mali zilizoachwa na marehemu baba yake.

Inadaiwa kuwa mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 54, alifanya tukio hilo usiku wa Septemba 23, 2024 na kisha kutelekeza mwili wa mama yake ndani ya chumba chake alichokuwa anaishi.

Mwili wa mama huyo ulikutwa ukiwa umelazwa kifudifudi huku shingoni kukiwa kumefungwa kipande cha kanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa jeshi hilo linamshikilia mwanaume huyo kwa mahojiano zaidi.

“Septemba 23, 2024 usiku wa saa 4, maeneo ya Uru Okaseni, mwanamke ajulikanaye kwa jina la Adela Dominick Mushi, aliuawa kwa kupigwa na kitu butu kichwani kisha kunyongwa kwa kutumia kipande cha kanga na mtoto wake aitwaye Nemes Dominic,” amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha mauaji hayo kinachunguzwa , lakini wawili hao walikuwa na ugomvi wa muda mrefu wakigombea mashamba na mali za marehemu.

Mwenyekiti wa kijiji asimulia

Akielezea tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Alphonce Mtaresi amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa jirani wa mama huyo walifika eneo la tukio na kuukuta mwili huo ukiwa chini chumbani kwake.

“Nilipokea taarifa asubuhi ya saa 4, kuna jirani alikuja ofisini akatupa taarifa ya kwamba kuna mama amefariki, tukatoka ofisini mimi na mtendaji, tukaenda nyumbani kwa huyo mama kweli tulikuta kafariki na mwili upo sakafuni,” amesema mwenyekiti huyo.

Pia, ameongeza: “Katika kuangalia mazingira ya tukio, ni kwamba huyu mama aliuawa kwa kupigwa shoka kwenye shavu moja la kushoto, karibu na jicho na shingoni kulikuwa na kanga kama vile amenyongwa, ni tukio la kusikitisha na kuumiza sana.”

Mwenyekiti huyo amesema Nemes  mara kadhaa amekuwa akimsumbua na kutishia kumuua mama yake, akitaka mali za marehemu baba yake.

“Mara nyingi nimekuwa nikisuluhisha migogoro ya huyu mama na mtoto wake, huyu mtoto tulishampeleka polisi zaidi ya mara sita kwa sababu alikuwa akimtishia mama yake kumuua, lakini changamoto ambayo mara nyingi ilikuwa ikionekana ni mambo ya mali,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema baada ya baba huyo wa familia kufariki na kuacha mali ikiwemo nyumba na mashamba, kijana huyo amekuwa akimsumbua mama yake akitaka urithi wa mali, jambo ambalo mama huyo alikuwa akimweleza kwamba hawezi kugawa bila ndugu zake wengine kuwepo, hivyo asubiri.

“Baada ya huyu baba wa familia kufariki na kuacha mali, sasa huyu kijana akawa anadai kwamba kuna sehemu ya shamba ambalo anataka mama yake ammilikishe na lengo alikuwa apate hicho kipande auze, sasa mama yake hakukubali, ndio hivyo imetokea kauawa,'”amesema mwenyekiti huyo

Vilevile, ametoa wito kwa vijana kuwapenda wazazi wao na kutambua umuhimu wao hapa duniani na sio kuwaua.

“Huyu mama alikuwa hana shida na mtu yeyote alikuwa na upendo na kila mtu, kwa kweli kifo chake kimetuumiza sana maana huyu kijana kamsumbua kwa muda mrefu,” amesema.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mawenzi kwa uchunguzi zaidi.

Related Posts