Kiungo wa Yanga, Aziz Andabwile amesema wanafahamu kilichowahi kuwakuta mkoani Mbeya, Yanga alipopoteza mechi zake dhidi ya Ihefu kwa misimu miwili mfululizo, hivyo watakuwa makini na tahadhari kubwa kufikia malengo.
Kwenye michezo miwili ya ugenini mkoani Mbeya, Yanga ilichapwa mabao 2-1 msimu wa 2022/23 na 2023/23 na imekuwa ni mechi ngumu kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ikiwa mkoani humo.
Yanga inashuka uwanjani leo kuanzia saa 10:15 jioni kuivaa Gen Gold ikiwa ni mchezo wake wa pili baada ya kumaliza michezo ya kimataifa na kufuzu makundi na Kocha Miguel Gamondi alisema anachokitaka ni pointi tatu na kama wapinzani wao wakijichanganya watatumia vilivyo nafasi kwenye mechi hiyo Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
KenGold ambayo hivi karibuni iliachana na kocha wake mkuu, Fikiri Elias na msaidizi wake Luhaga Makunja, haijashinda wala kupata sare tangu msimu uanze.
Yanga imeshuka dimbani mara saba kwenye michuano yote na kushinda mechi zote. Imepachika mabao 24 na kuruhusu moja pekee. KenGold, mechi nne za ligi ilizocheza msimu huu imepoteza zote ikifunga mabao mawili na kuruhusu nane. Inashika nafasi ya mwisho katika msimamo.
Ni mechi yao ya kwanza dhidi ya timu kongwe za hapa nchini. KenGold ambayo hivi sasa inanolewa na Kocha Jumanne Charles akisaidiana na Aswile Asukile wana kazi ya kufanya kuizuia Yanga lakini pia kuisaka pointi ya kwanza ligi kuu.
Timu hiyo yenye maskani yake Chunya mkoani Mbeya, inamtegemea zaidi mshambuliaji wake Joshua Ibrahim ambaye ndiye aliyefunga mabao mawili waliyonayo kikosini hapo.
Mabeki wao akiwamo Ambukise Mwaipopo, Asanga Stalon, Makenzi Kapinga, Salum Iddrisa, Bila Amin, Martin Kazila na Charles Masai ambao wameonekana kucheza mechi zilizopita, wana kazi kubwa ya kuizuia safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Yanga imekuwa na kawaida ya kuwatumia viungo zaidi katika kutengeneza na kufunga mabao, wana rekodi nzuri Sokoine kwani mechi tano za mwisho ilizokwenda kucheza hapo na timu tatu tofauti, haijapoteza hata moja.
Mara ya mwisho Yanga kwenda Sokoine ilikuwa Februari 11 mwaka huu ambapo iliichapa Tanzania Prisons mabao 1-2 yaliyofungwa na Clement Mzize dakika ya 8 na Pacome Zouzoua (dk 45+3). Tanzania Prisons walifunga kupitia Jeremiah Juma dakika ya 64. Ukiachana na hilo, Yanga katika mechi hizo tano za mwisho Sokoine, imetoka sare mbili na zote ni dhidi ya Mbeya City.
Kocha Gamondi amesema; “Mimi kiu yangu ni Yanga kupata pointi tatu hata kwa bao moja ni sawa, ila kama tutapata nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo na itakuwa nzuri zaidi, nimewaandaa vyema wachezaji wangu,” alisema Gamondi na kuongeza kuwa hana hofu yoyote kwani wachezaji wake wana uzoefu na uwezo binafsi.
Kocha wa timu hiyo, Jumanne Charles amesema baada ya kuisoma Yanga amegundua ubora wao ni eneo la kiungo, mipira ya kushtukiza na dakika za mwanzo.
Amesema kutokana na hilo, watadhibiti vizuri zile pasi za Yanga na mikimbio akieleza kuwa Mudathir Yahya anamfahamu vyema kwani alishakuwa naye wakati akiinoa Singida Black Stars, hivyo atamtuliza.
Straika wa timu hiyo, Joshua Ibrahim (pichani) ametamba kuwa mabeki wa Yanga wakiongozwa na Ibrahim Bacca wanapitika hivyo kiu yake ni kuwafunga vigogo hao.