Baada ya Simba, Mussa ataka heshima Mashujaa

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Mohamed Mussa anayekipiga kwa sasa Mashujaa, amesema akili yake ni kusaka heshima katika Ligi Kuu Bara na kwamba anaona msimu huu anarudi na moto.

Akiwa Simba iliyomsajili Januari 2023 kutoka Malindi ya Zanzibar, mchezaji huyo alikiwasha mechi moja tu ya FA dhidi ya Coastal Union aliyoshangilia hadi kuvua tisheti, ambapo msimu uliopita akatemwa kikosini.

Ingawa bado hajaanza kufungua akaunti ya mabao Mashujaa, Mussa alisema kitendo cha kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara anaona ndiyo silaha pekee ya kufunga mabao na kazi yake kuwa bora.

“Nina furaha kujiunga na Mashujaa, hakuna timu inakosa ushindani wa namba, ila nina imani kubwa msimu huu unakwenda kunipa hatua nyingine katika maisha yangu ya soka,” alisemaa Mussa na kuongeza:

“Naendelea kujituma katika mazoezi ili kumshawishi kocha kuniamini katika kikosi chake. Jambo kubwa kwa mchezaji ni kupata nafasi ya kucheza mengine yanakuwa ni rahisi kuyatimiza, kwani ni ngumu usipocheza kufanya kile kitakachotimiza malengo.”

Mashujaa imekusanya pointi nane katika Ligi Kuu Bara hadi sasa baada ya kucheza michezo minne.

Related Posts