Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, imemuachia huru babu (ambaye kwa sababu za kimaadili na kisheria zinazotaka mwathirika asitambuliwe kwa namna yoyote, tunahifadhi jina lake), aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa madai ya kumbaka mjukuu wake.
Mkazi huyo wa eneo la Kantalamba Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, alidaiwa kumbaka mjukuu wake mwenye umri wa miaka 12, kati Februari hadi Machi 2020.
Rufaa hiyo ya jinai namba 13,275 ya mwaka 2024 ilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, katika kesi ya jinai namba 79 ya mwaka 2020.
Uamuzi wa rufaa hiyo ulitolewa Septemba 23, 2024 na Jaji Thadeo Mwenempazi ambaye baada ya kupitia hoja za rufaa na mwenendo wa shauri hilo, alibaini shitaka hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Babu huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, kwa kosa moja la ubakaji ambapo alidaiwa kumfanyia kitendo hicho mjukuu wake katika kipindi tajwa hapo juu.
Baada ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, ilimtia hatiani babu huyo na kumuhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Baada ya adhabu hiyo babu huyo hakuridhika nayo na kukata rufaa Mahakama Kuu akiwa na sababu tano ikiwemo upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake.
Nyingine ni Mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kumtia hatiani na kumuhukumu bila kuzingatia kwamba kulikuwa na mkanganyiko wa umri wa mwathirika ambapo ilidaiwa ana miaka 11, lakini mahakamani ilidaiwa ana miaka 12, jambo linaloleta mashaka mbele ya sheria.
Nyingine ni Mahakama hiyo ilikosea kisheria kumtia hatiani na kumuhukumu kulingana na shahidi wa upande wa mashitaka, wakati haikuona kuwa mashahidi wote wa mashitaka hawakuapishwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, babu huyo alijitetea yeye mwenyewe bila kuwakilishwa na alikubali sababu zake za kukata rufaa na kuiomba Mahakama imuachie huru, huku upande wa mashitaka ukiwakilishwa na wakili wa Serikali Scolastica Mwacha.
Akijibu hoja hizo za rufaa, Wakili Scolastica alidai vipengele vya kosa hilo vilithibitishwa na kuwa wakati mrufani huyo anatekeleza vitendo hivyo alijua mwathirika huyo ni mjukuu wake.
Alisema upande wa mashitaka ulithibitisha kutendekea kwa kitendo hicho, kwani katika ukurasa wa 10 wa mwenendo wa kesi, aya ya tano, mwathirika huyo alieleza jinsi mrufani alivyombaka.
Wakili huyo alisema hilo pia lilithibitishwa na Fomu ya Polisi namba tatu (PF3) ambayo ilionyesha kuwa mwathirika huyo hakuwa bikira.
Kuhusu hoja ya mashahidi kutoa ushahidi bila kuapishwa, wakili huyo alidai kuwa mwathirika wa tukio hilo aliyekuwa na umri wa miaka 11 ndiye hakuapishwa na kwa mujibu wa kifungu cha 127 (2) cha Sheria ya Ushahidi, mwathirika ameainishwa kama mtoto wa umri mdogo.
Amesema kutokana na sababu hiyo hakuwa na wajibu wa kuapa, hivyo alitakiwa kuahidi kusema ukweli kila wakati na kuwa mashahidi wengine wote ambao ni shahidi wa pili, tatu na nne waliapa kabla ya kutoa ushahidi.
Jaji Mwenempazi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, suala la kuzingatia ni iwapo kosa ambalo mrufani huyo alishitakiwa nalo na kutiwa hatiani lilithibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Jaji huyo alisema ni wazi mwathirika huyo katika ushahidi wake aliieleza Mahakama kuwa alikuwa akiishi na babu na bibi yake, ambapo bibi huyo alidaiwa kumfukuza mumewe kutokana na malalamiko ya mjukuu wake.
Ilidaiwa matukio hayo ya ubakaji yalikuwa yakitokea wakati bibi huyo amekwenda shambani ila bibi huyo hakuweza kuitwa mahakamani kutoa ushahidi, kwani alifariki wakati kesi inasikilizwa.
“Pia nimeangalia mwenendo wa kesi mahakamani, mashahidi wote walitoa ushahidi kwa kiapo isipokuwa mwathirika huyo, ambaye aliahidi kusema ukweli kulingana na matakwa ya sheria kutokana na umri wake,” alisema Jaji.
Jaji huyo alisema ana mashaka iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa kwa kiwango kinachohitajika, na wasiwasi wake ni iwapo inawekezanaje matukio hayo yaliendelea bila kujulikana na watu wa karibu.
“Swali lingine ni je, bibi (kwa sasa ni marehemu) mke wa mrufani angempiga vipi mjukuu wake kuwa mwongo baada ya kuripoti kwake na kisha kumfukuza mumewe nyumbani kulingana na kosa lililoripotiwa?
“Kwa nini shahidi mwingine (jirani) aliyeenda kuripoti taarifa hizi hakuitwa kutoa ushahidi wake kwa kile alichoelezwa na mwathirika wa tukio hili? alisema.
Jaji alisema anaelewa chini ya kifungu cha 127(6) cha Sheria ya Ushahidi, ushahidi wa mwathirika huyo unaweza kutosha kutoa hatia ya mrufani, lakini kwa kuzingatia mapungufu na au mashaka yaliyotolewa hapa juu, naona kesi haijathibitishwa kwa kiwango kinachohitajika na sheria.
“Kwa sababu, rufaa inaruhusiwa, hukumu ya mrufani inatenguliwa na ninaamuru mrufani aachiwe mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali,”aliamuru Jaji.