DIVISHENI YA MIPANGO OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAENDESHA MAFUNZO MAALUMU YA UAANDAJI WA MPANGO NA BAJETI.

Na Mwandishi wetu

Divisheni ya Mipango Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendesha mafunzo ya uandaaji mpango na bajeti na utekelezaji wake kwa maafisa bajeti kutoka Divisheni, Vitengo na Ofisi za Mikoa za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mafunzo hayo ya siku 3 yanafanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 25 hadi 27 Septemba, 2024.

Mafunzo hayo yameandaliwa na kuendeshwa na Divisheni ya Mipango Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Divisheni ya Mipango Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Buji Bampebuye amewakaribisha washiriki wote wa mafunzo hayo na kueleza kuwa lengo kubwa la kufanya mafunzo hayo ni kuwajengea na kuwaongezea uwezo Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika masuala yanayohusu mipango na bajeti pamoja na namna bora ya kutekeleza Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa Taasisi.

Aidha, Mkurugenzi wa Divisheni ya Mipango ameendelea kueleza kuwa katika mafunzo hayo washiriki watapata kufahamu namna ya kupangilia na kuandaa bajeti, kuandaa na kutekeleza Mpango Kazi na mtiririko wa fedha, kuandaa Mfumo wa Mapato na Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) pamoja na ufutailiaji na udhibiti wa bajeti.

“Mafunzo haya kwa mwaka huu tumeona tuyafanye kwa kuwahusisha wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ili waje kutuongezea ujuzi zaidi, nawaomba muwe huru kuuliza maswali kuhusu suala lolote linalohusu bajeti, mjitahidi kujikita kwenye kuhusianisha Mfumo wa Mapato na Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) na Mpango Mkakati (Strategic Plan).” Amesema Mkurugenzi wa Mipango.

Kwa upande wake Bw. Shedrack Ndaile ambaye ni Mtaalamu wa masuala ya bajeti kutoka Wizara ya Fedha amefanya wasilisho lililohusisha mada ya uundaaji wa bajeti, uidhinishaji wa bajeti, utekelezaji wa bajeti, ufuatiliaji na udhibiti wa bajeti pamoja na Mfumo wa Mapato na Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF), ambapo aliwaeleza kwa akina mchakato wa uandaaji wa bajeti unavyofanywa na Serikali, na baadaye katika ngazi ya Taasisi.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi anayesimamia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jijini Arusha Bi. Veritas Mlay ameishukuru Divisheni ya Mipango kwa kuandaa mafunzo maalumu ya bajeti, kwa kuwa yatawasaidia maafisa bajeti kuongeza uelewa kwenye masuala mbalimbali yanayohusu mipango na bajeti, hivyo kuongeza ufanisi katika uaandaji na utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mafunzo haya yatatuimairisha katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti katika ngazi ya Divisheni, Vitengo, Ofisi za Mikoa, na naamini baada ya kumalizika kwa mafunzo haya tutaongeza uelewa katika masuala haya ya mipango na bajeti”. Amesema Wakili wa Serikali Mwandamizi.




Related Posts