EAGLE inazidi kuonyesha makali katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza (MRBA), baada ya kuifunga CUHAS kwa pointi 71-44 katika Uwanja wa Mirongo mjini humo.
Ushindi kwa timu hiyo ni wa tatu mfululizo kwani katika mchezo kwanza iliifunga Young Profile kwa pointi 49-43 na ule wa pili ikaifunga Sengerema Hoopers pointi 52-49.
Katika mchezo huo, Ian Musira wa Eagle alifunga pointi 19, akidaka mipira ya ‘rebound’ mara 10 na kutoa asisti mara mbili. Nyota wa Young Profile, Kizami Kizami alifunga pointi nane na kutoa asisti tatu.
Katika mchezo mwingine uliochezwa uwanjani hapo Young Profile iliifunga Sengerema Hoopers kwa pointi 41-31.
Wakati huo huo TBT imeifumua Spide kwa pointi 69-40 katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Kigoma iliyoanza kwenye Uwanja wa Lake Side mjini humo.
Katibu mkuu wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Kigoma, Aq Qassim Abasi alisema timu tisa zinashiriki katika mashindano hayo.
Alitaja kuwa ni Kibondo, Kasulu Heat, TBT, Lake Side, Spide na Wavuja Jasho, huku upande wa wanawake ni Lake Side Queens, Tanganyika Queens na Spide Queens. Mashindano ya kikapu mkoani Kigoma yalichelewa kuanza kutokana na sababu mbalimbali, ambapo mara kwa mara yalikuwa yakiahirishwa.