EDGAR William ni miongoni mwa maingizo mapya kwenye kikosi cha Fountain Gate msimu huu na tangu msimu huu umeanza tayari ameonyesha ni mshambuliaji hatari kwa kufumania nyavu za wapinzani jambo linalompa kiburi kocha wa timu hiyo, Mohamed Muya.
Nyota huyo ameingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Muya huku akicheza katika nafasi mbalimbali uwanjani ikiwemo ya winga wa pembeni na mshambuliaji wa kati akishirikiana na straika mwenzake, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ aliyetoka KVZ ya Zanzibar.
Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa mchezaji huyo ambaye licha tu ya kutoimbwa kama ilivyokuwa kwa wengine ila kazi yake inaonekana uwanjani.
Kabla ya kujiunga na kikosi cha Fountain Gate msimu huu, Edgar alishaonyesha kwamba anajua kufunga jambo lililowavutia mabosi wa timu hiyo kumsajili, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na KenGold ya jijini Mbeya aliyoipandisha daraja.
Nyota huyo msimu uliopita akiwa na KenGold aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 21 kwa msimu mzima ikiwa ni rekodi mpya kwani kabla ya hapo haijawahi kutokea mshambuliaji aliyefunga idadi kubwa kiasi hicho.
Tangu msimu wa 2017/2018, rekodi kubwa ya kufunga mabao ilikuwa ikishikiliwa na mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo aliyefunga mabao 18 msimu wa 2022/23 ingawa idadi hiyo ilivunjwa na Edgar na kujitengenezea ufalme wake binafsi.
Mbali na ufungaji bora wa Championship, Edgar ameshinda pia Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Championship msimu uliopita baada ya kuwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Boban Zirintusa wa Biashara United aliyetimkia Tusker ya Kenya.
Mshambuliaji huyo anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amezipandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu Bara akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021/22 na KenGold msimu huu.
Uwepo wake kikosini unamfanya kutishia baadhi ya nafasi kwa nyota wengine akiwemo aliyekuwa winga wa Namungo na Mtibwa Sugar, Kassim Haruna ‘Tiote’, ambaye tangu msimu umeanza anapata wakati mgumu wa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.
Edgar alianza kujitafuta upya baada ya kupitia maisha magumu akiwa na kikosi cha Kagera Sugar, ambapo baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara aliamua kuomba kuondoka ili kunusuru kipaji chake na ndipo aliporudi KenGold kujitafuta.
Tayari kocha wa Fountain Gate, Muya ni kama vile ameshajua namna ya kumtumia mchezaji huyo akiwa sambamba na mshambuliaji mwenzake, Seleman Mwalimu ambao wote wametengeneza safu bora ya ushambuliaji wakiwa na kikosi hicho.
Gomez aliyesajiliwa na Fountain msimu huu akitokea KVZ inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), msimu uliopita aliibuka mfungaji bora, ambapo alifunga mabao 20 na kuchangia mengine saba ‘(asisti), katika michezo 27 aliyocheza kati ya 30 kwa msimu mzima.
Nyota hao kwa pamoja wameshafunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara hadi sasa kila mmoja wakiwa wamechangia sita kwa ujumla kati ya tisa yaliyofungwa na kikosi kizima kwenye michezo mitano ambayo wamecheza jambo linaloonyesha wazi ni hatari kwa kufunga.
Msimu huu, Edgar ameonyesha uwezo mkubwa katika kikosi hicho na licha tu ya kufunga akitokea pembeni au mshambuliaji wa kati ila moja ya mambo makubwa ambayo yameongezeka kwake ni jinsi anavyoweza kucheza katika nafasi tofauti uwanjani.
Katika michezo yao ya hivi karibuni, nyota huyo ameonekana akishambulia pindi timu inaposhambulia na pia ameonekana akirudi nyuma kusaidia ulinzi na kufuata mipira, kitu ambacho kimekuwa ni kivutio kikubwa kinachosababisha kuendelea kuaminiwa katika kikosi cha kwanza.
Mara kadhaa katika michezo migumu, Egdar amekuwa akirudi nyuma kusaidiana na viungo mwengine akiwemo, Abdallah Kulandana aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu pia akitokea Mlandege ya Zanzibar, hali inayoifanya timu hiyo kuwa bora hadi sasa.
Akizungumzia mwenendo huo, Edgar anasema, siri kubwa ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na ushirikiano na wachezaji wenzake.
“Ili tufanye vizuri ni lazima ushirikiano uwepo kwa sababu hiyo ndio siri kubwa ya kufanikiwa, ni kweli nimefanya vizuri hadi sasa ila kwangu naona nina deni kubwa la kulipa, wengi wana matumaini na mimi hivyo ni changamoto kwangu kikosini.”