WAKATI Simba ikijiandaa na kucheza ugenini kesho dhidi ya Azam FC, kocha wa kikosi hicho Fadlu David amefunguka kuwa anazo taarifa zote za wapinzani hao huku mastaa wajitapa hadharani juu ya pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja Zanzibar.
Simba inakwenda kucheza mchezo wa tatu wa ligi, huku Azam ikiwa inaingia katika mechi ya tano, huku rekodi zikionyesha mara ya mwisho zilipokutana Azam ililala 3-0 baada ya awali kutoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa CCM Kirumba, Mwanza. kutoboa mbele ya Wekundu hao.
Timu hizi zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu zote zikiwa na makocha wapya, Azam ikiwa na Rachid Taoussi na Simba ni Fadlu Davids, lakini zote zikiwa hazijaruhusu bao lolote katika mechi za ligi ilizocheza hadi sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha huyo amesema, Azam ina kikosi kizuri chenye timu bora yenye ushindani.
Aidha amesema, kitu kikubwa anachowaza ni mechi zilivyofululiza kwani wanatoka Zanzibar na kwenda Dodoma ndani ya wiki moja.
“Tumetoka kwenye mchezo mgumu hivyo tunachofanya kwa sasa ni kuendelea na mazoezi mepesi tu ya viungo.
Kuhusu Azam tunakwenda kwa kuwaheshimu kwa sababu wana kikosi kipana, lakini tunaangalia mbinu zao kupitia mikanda na ninaamini timu yangu itafanya vizuri.”
“Tutacheza kwenye nyasi bandia hivyo sio rahisi sana kwa upande wa wachezaji wetu ila haimaanishi kama hatutatoboa,” amesema Fadlu.
Beki Shomari Kapombe amesema, sio yeye tu anaetaka timu ipate ushindi bali hata kocha wao.
Aidha amesema, kocha wao amekuja muda mfupi uliopita ila ameweza kubadili kikosi chao kwa haraka na kukipa mafanikio makubwa, hiyo tu inatoa matumaini ya picha ijayo.
“Ushindani wa ligi umezidi kuongezeka, kwani hakuna timu ndogo kutokana na klabu zimesajili wachezaji wazuri wenye viwango.
Hivyo kwetu kila hatua tunayopiga kocha anatufundisha kuwa na bidii zaidi na kurekebisha makosa ya mechi zilizopita ili mchezo ujao waweze kufanya makubwa, hivyo ushindi ni uhakika,” amesema Kapombe, huku nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema, mechi dhidi ya Azam watakwenda kwa kujiamini na kufuata mbinu za kocha alizowapa mazoezini na kwa uzoefu.
“Kuhusu wachezaji wapya ambao hatujawahi kucheza nao tutaangalia mikanda ya mechi za msimu huu ili tuweze kuwajua na kujipanga kupambana nao.
“Malengo yetu msimu huu ni kuchukua ubingwa ndio maana tumeanza ligi kwa kasi kubwa na kufunga mechi mbili na tunaamini Azam hata pindua rekodi hiyo.”
Simba itashuka ugenini kesho, Septemba 26 katika Uwanja wa Amaan Complex uliopo Zanzibar, mchezo utakaochezwa saa 2:30 usiku.