Historia ya mvutano maandamano kati ya Polisi, upinzani Tanzania

Katika nchi nyingi zinazoendelea, uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya upinzani umekuwa wa kusuasua kutokana na mivutano ya kisheria na kikatiba, hasa linapokuja suala la maandamano.

Hali hiyo ipo pia Tanzania, Jeshi la Polisi na vyama vya upinzani, kihistoria, wamekuwa na uhusiano usioridhisha ambapo kila mmoja anatumia kifungu kwenye Katiba kuhalalisha anachotaka kukifanya.

Vyama vya siasa vinaeleza kutumia haki yao ya kikatiba na ya kisheria ya kufanya maandamano ya amani baada ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, saa 48 kabla ya kufanya maandamano hayo au mkutano wa hadhara.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi nalo limepewa nguvu, kwamba, linapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, linaweza kuzuia kufanyika kwa maandamano husika ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Kutokana na kutoaminiana, pande hizo mbili zimekuwa zikiingia katika malumbano ambayo yamekuwa yakisababisha madhara kwa waandamanaji na pia hata watu wengine wasiojihusisha na maandamano hayo.

Wakati maandamano ya Chadema yalikuwa yafanyike Septemba 23, mwaka huu, yakidhibitiwa na Jeshi la Polisi, siyo mara ya kwanza kwa jeshi hilo na vyama vya upinzani kukwaruzana na kusababisha madhara.

Maandamano kadhaa yalifanyika miaka ya nyuma na kusababisha watu kujeruhiwa na polisi na wengine kuuawa walipokuwa wakijaribu kuyazuia, huku shughuli za kiuchumi zikisimama kutokana na kukosekana kwa utulivu.

Chama cha Wananchi (CUF) kilipokuwa chama kikuu cha upinzani, kilikabiliana na Jeshi la Polisi katika maandamano yao. Chadema, pia, kikiwa chama kikuu cha upinzani, kimekabiliana na jeshi hilo mara kadhaa.

Maandamano ya Januari 2001

Maandamano makubwa katika historia ya Tanzania, yanatajwa kuwa yale yaliyofanyika mwaka 2001 huko Zanzibar, baada ya wanachama wa CUF kuandamana na kukabiliana na Jeshi la Polisi, matokeo yake kusababisha vifo vya watu na majeruhi.

Kutokana na malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofanyika huko Zanzibar Oktoba 2000, CUF kiliitisha maandamano nchi nzima Januari 27, 2001 kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Ripoti ya Human Rights Watch inaeleza kwamba vikosi vya usalama vya Serikali ya Tanzania vikiongozwa na Jeshi la Polisi, viliyakandamiza na kuyavunja maandamano ya kisiasa yaliyoitishwa huko Zanzibar kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Jeshi la Polisi likisaidiwa na askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) walidhibiti na kukabiliana na waandamanaji ambapo waliwakamata na kuwapiga watu walioandamana visiwani humo.

Watu kadhaa waliuawa kwenye makabiliano hayo, ambapo HRW ilikadiria kuwa watu 35 waliuawa na wengine kujeruhiwa. Wazanzibari wengine 2,000 walidaiwa kukimbilia nchi jirani ya Kenya.

CUF pia ilikuwa inadai mabadiliko ya Katiba. Katika hatua iliyopokelewa kwa furaha Januari 2002, Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa alitangaza kuunda Tume ya Uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama huko Zanzibar mwaka 2001.

Akizungumza kwenye mkutano wa kumbukizi ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alitahadharisha madhara yaliyotokea mwaka 2001, hivyo alishauri kuwepo kwa mazungumzo baina ya pande zinazokinzana.

“Tukienda kwenye uchaguzi, bila makubaliano, zitatokea vurugu, mambo haya ya uchaguzi yanasababisha vurugu. Yaliyotokea mwaka 2001 bado yanapita kichwani, nisingependa yatokee tena,” alisema kiongozi huyo mstaafu.

Januari 27, 2015, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam liliwakamata wanachama wa CUF 32, akiwemo Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kufanya maandamano ambayo polisi walisema hayakuwa halali.

Awali, polisi ilizuia maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa na chama hicho ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 14 tangu kufanyika kwa mauaji ya wananchi wa Zanzibar na Bara.

Profesa Lipumba na viongozi wenzake walikuwa wakienda viwanja vya Zakhem, Mbagala kuwatawanya kwa amani wafuasi wa CUF, baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa mapema ya kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara uliopangwa kwa ajili ya kufanya maadhimisho hayo.

Maandamano hayo yalipangwa kuanzia Temeke Mwisho na kuishia Mbagala Zakhem, wilayani Temeke ambako chama hicho kilikuwa na nguvu kubwa.

Februari 2018, wafuasi wa Chadema na viongozi wao walifanya maandamano kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kudai fomu za mawakala wao, wakidai walizuiwa kusimamia uchaguzi mdogo katika jimbo hilo.

Wakati wa maandamano hayo, Jeshi la Polisi lilitumia mabomu ya machozi ambapo inadaiwa mwanafunzi mmoja aliuawa kwa risasi kwenye maandamano hayo yaliyosambaratishwa na polisi.

Akwilina Akwilini alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye daladala eneo la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam, wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.

Katika maandamano ya Januari 24, mwaka huu, viongozi wa Chadema waliandamana kwa kujitokeza katika maeneo yaliyobainishwa ya Mbezi Luis, Buguruni na Kariakoo kuanzia saa 12 asubuhi. Hata hivyo, maandamano haya yalilindwa na polisi.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema lengo la maandamano hayo lilikuwa kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni na kutaka Serikali itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana na kupanda gharama za maisha kwa Watanzania.

Maandamano ya Septemba 23, ni mwendelezo wa maandamano ya chama hicho, yakilenga kupinga matukio ya watu kutekwa na kuuawa, hususan viongozi wa Chadema ambao, baadhi wanadaiwa kutekwa na wengine kuuawa.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mgongano kati ya polisi na upinzani nchini, Kamanda wa Polisi mstaafu, Jamal Rwambow anasema hakuna sababu ya watu kuendelea kugombana na kutoelewana katika vitu ambavyo havileti taswira nzuri kwa nchi.

“Busara zinapaswa kutumika lakini kuna mengine nje ya pazia hayazungumzwi, kwamba nia inakuwa si rafiki au kutaka kuona nani mbabe zaidi ya Polisi au Polisi akipiga kirungu basi kila mtu amejiandaa na kamera yake dunia nzima ione.

“Ukiwa na nia nzuri ya kufanya jambo jema, hakuna wakati Polisi wanaweza kuzuia na sitaki kuamini kama kuna mgongano kati ya Polisi na Chadema. Lakini, nadhani pande hizo zinaweza kukaa wakaona njia nzuri ya kufanya kwa sababu tangu mwaka 1992, Sheria ya Vyama vya Siasa iliporuhusu mfumo wa vyama vingi, hiyo hali imekuwepo,” anasema.

Rwambow, aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, anasema baada ya kuanzishwa kwa sheria hiyo ya vyama vingi, walikuwa wanatumia muda mwingi kuelekezana na viongozi wa upinzani, ingawa kulikwepo na hali ya ukaidi kwa kiasi fulani.

“Walipokuwa wanakaidi kutaka kuonyesha wao ni bora zaidi, migongano ilikuwa inatokea, lakini tulikuwa tunakaa na kuzungumza nao, ilikuwa viongozi wa Polisi maeneo mbalimbali wakati ule hata kanda hazijaanzishwa, wanakutana na viongozi wa upinzani kuelekezana, hii njia inaweza isiwe nzuri, ni mambo yanayozungumzika,” anasema.

Anasema hakuna jambo ambalo linashindikana kwa kuwa vyama vya upinzani ni Watanzania na wana haki sawa kama wengine. Hivyo, hakuna sababu ya kuzozana kila siku na hata Polisi wanalijua hilo.

“Ifikie hatua watu waaminiane, kama huwaamini Polisi wanaolinda raia, hapo sasa mnaonyeshana ubabe na hatuwezi kwenda kwa ubabe na madhara yake yanakuwa si mazuri, labda inaweza kuwa faida kwa mwingine, akifanya hivi itaonekana ametimiza jukumu ambalo wengine hawalijui,” anasema.

Anasema kipindi wanafanya kazi, walikuwa wanaongea na viongozi wa vyama vya upinzani, ingawaje kwa sasa kiongozi wa Jeshi la Polisi akienda kuongea na kiongozi fulani wa upinzani inakuwa kama kosa.

Anasema kila mtu ana haki yake, lakini ikionekana upande mmoja unajiona wenye haki kuliko mwingine, tatizo linaanzia hapo.

“Hata Polisi hawatakiwi kuonekana wana haki kuliko wengine na wanaohitaji maandamano hawahitaji kuona wao wana haki zaidi, bahati mbaya imefikia hatua hata zile taratibu za msingi za kuomba maandamano zinakiukwa.

“Maandamano mengi ukifuatilia yanaombwa kwa njia ya vyombo vya habari, mtu anaita press conference (mkutano na wanahabari) na kueleza nitafanya maandamano kwa malengo fulani na atatumia njia kadhaa, wakati fulani hata wanapojibiwa mahali ambapo hakuna maombi hayo, kwa maoni yangu ni matatizo,” anasema.

Anabainisha kuwa sheria ya kufanya maandamano inaeleza wazi kuwa inatakiwa katika muda wa saa 48 kabla ya kuandamana, watoe taarifa kwa Mkuu wa Polisi mwenye mamlaka ya eneo wanalohitaji kufanya shughuli hiyo.

“Mkuu wa Polisi akipokea taarifa anatakiwa kufanya mambo matatu; kwanza anaweza kukaa kimya au akajibu kwa njia ya kuelekeza kukutana kwao na kuona namna gani njia wanazohitaji zinaweza kutumika au vinginevyo,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Bubelwa Kaiza anasema Polisi na vyama vya siasa havina mamlaka yoyote isipokuwa wananchi.

“Kwa bahati mbaya raia hawajielewi wala kujitambua na wamefanywa wasijielewe wala kujitambua na imekuwa rahisi kwa kila upande kujichukulia mamlaka ya raia na kudhani wanawakilisha raia na kinachogombewa ni hicho, nani awakilishe raia,” anasema.

Kaiza anasema hata kinachoendelea kwa sasa, hoja kubwa ni usalama wa raia na wala si ajenda ya vyama vya siasa, ni kwa watu wote, kwani kuna waliotekwa au kuuawa.

Alisema iwapo raia wangekuwa na ufahamu na kukaa katikati yao, Polisi wangetii na raia wangewaunga mkono upinzani.

“Kwa kuwa raia hawajitambui, ndiyo maana yamekuwa matatizo yanayojirudia kila mwaka tangu uhuru,” anasema Kaiza.

Kwa upande wake, mwanaharakati Hellen Kijo-Bisimba anasema njia sahihi ya kufanyika kwa pande hizo zinazovutana ni kufuata sheria, huku akieleza Jeshi la Polisi halizingatii takwa hilo la kikatiba.

“Jeshi la Polisi, kama raia wanataka kufanya maandamano, wanatakiwa kutoa taarifa polisi, maana yake wanakuwa wameandaliwa kuimarisha ulinzi ambayo ni kazi yao na wana uwezo huo, badala yake Polisi mara zote wanatafuta visingizio ili wazuie,” anasema.

Related Posts