Keyekeh afichua jambo Ligi Kuu Bara

KIUNGO wa Singida Black Stars, raia wa Ghana, Emmanuel Keyekeh amesema licha ya kuanza vizuri msimu huu na kikosi hicho, lakini bado ana kazi kubwa ya kufanya, huku akiweka wazi siri ya mwenendo mzuri na timu hiyo ni ushirikiano uliopo kwao.

Nyota huyo amejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea FC Samartex ya kwao Ghana ambapo licha ya kucheza msimu wake wa kwanza na timu hiyo, ila tayari ameonyesha ni mchezaji muhimu wa kuangaliwa kutokana na kiwango kizuri anachokionyesha.

“Nahitaji kufanya zaidi ya sasa, ni mapema sana kwa sababu bado tuna michezo mingi iliyokuwa mbele yetu, siri kubwa ni ushirikiano kwani siwezi kufanya vizuri bila ya wenzangu, tuna kikosi bora cha kushindana na kila mpinzani,” amesema.

Keyekeh aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwemo, Asante Kotoko, Karela United na UniStar Soccer Academy zote za kwao Ghana amesema Ligi Kuu Bara ni ngumu tofauti na alikotoka ingawa kadri anavyozidi kucheza anaendelea kuizoea taratibu.

“Sio rahisi kwa sababu ushindani ni mkubwa na kila timu ina wachezaji wazuri, kikubwa ni kuhakikisha tunaendeleza umoja wetu katika kila mchezo tunaocheza ili tufikie malengo tuliyojiwekea, uwezo wa kuchukua ubingwa tunao japo ni mapema.”

Nyota huyo anashikilia rekodi ya mchezaji wa Ligi Kuu Bara aliyefunga bao la mapema zaidi hadi sasa akiwa na timu hiyo ambapo alifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Pamba Septemba 17, alipofunga sekunde ya 19, wakati Singida Black Stars iliposhinda kwa bao 1-0.

Pia amehusika na mabao matatu ya Singida katika Ligi Kuu Bara hadi sasa ambapo amefunga mawili na kuchangia moja kati ya saba yaliyofungwa na kikosi kizima, huku akishinda tuzo ya mchezaji bora mara tatu kwenye michezo yake minne aliyocheza.
 

Related Posts