Madina apigia hesabu Morocco | Mwanaspoti

MCHEZA gofu mahiri wa Tanzania, Madina Iddi anajiandaa na mashindano ya Afrika ya mchezo huo yatakayofanyika Agadir, Morocco, Novemba mwaka huu.

Madina ambaye ameibuka mshindi katika viwanja mbalimbali vya gofu Afrika akitwaa mataji manne na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kitimu, alisema amewapania wenyeji Morocco waliiondoa nchini wakiwa nafasi ya pili, huku Tanzania ikimaliza ya tatu licha ya kuwa ni mwenyeji wa mashindano haya mwaka 2022.

“Ilituuma sana, kwa hiyo na sisi tumepania kulipiza kisasi kwao Agadir yatakakofanyika mashindano ya mwaka huu,” alisema Madina baada ya Rais wa Chama cha Gofu ya Wanawake nchini (TLGU), Queen Siraki kutangaza timu ya Taifa itakayokwenda Morocco.

Wengine waliochaguliwa ni Hawa Wanyeche wa Dar es Salaam na Neema Olomi wa Arusha, huku Madina akiwa ndiye tegemeo kuu la nchi.

Madina ni Mtanzania wa kwanza kushinda ubingwa wa  Afrika kwa wachezaji binafsi baada ya kumshinda Mwafrika ya Kusini mwaka 2018.

Tangu kuasisiwa kwa mashindano ya Afrika mwaka 1992, ni Madina na Mkenya Rose Naliaka pekee, wana Afrika Mashariki walioshinda taji la Afrika kwa mchezaji binafsi.

Mbali ya kufanya vizuri katika mashindano ya Tanzania Ladies Open, jijini Arusha, Madina alisema kushinda mataji manne katika mashindano ya nje ya nchi yaliyofanyika Ghana, Zambia, Kenya na Uganda kumempa ari ya kufanya vizuri katika mashindano ya bara zima  kwa sababu yamemfanya pia aboreshe ujuzi wake katika gofu.

Madina aliuanza msimu kwa kushinda Ghana Ladies Open na baadaye kutwaa taji la Zambia Ladies kabla ya kutwaa mawili Uganda.

Yakijulikana kama All Africa Golf Challenge Trophy, mashindano ya mwaka huu yatafanyika mjini Agadir, Morocco kuanzia Novemba 28 hadi 30.

Katika mashindano ya mwisho jijini Dar es Salaam  mwaka 2022, Afrika Kusini iliibuka washindi wa jumla baada ya kupiga mikwaju 444, ikifuatiwa na Morocco iliyorudisha mikwaju 449 na Tanzania kumaliza nafasi ya tatu kwa jumla ya mikwaju 453.

Related Posts