PAMOJA na matokeo ya sare kuiandama Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata ameipongeza beki yake kwa kutoruhusu bao lolote, huku akiwafungia kazi mastraika.
Maafande hao wameandamwa na mzimu wa sare mfululizo katika michezo minne waliyocheza ikiwa hawajafunga wala kufungwa bao, jambo lililomuamsha Makata kuja kivingine.
Timu hiyo inatarajia kuwa uwanjani kuwakabili Namungo, mchezo utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi ukiwa wa raundi ya tano katika Ligi Kuu.
Makata alisema licha ya ugumu walioanza nao, lakini anaona sehemu ya beki haina makosa japokuwa tatizo lipo kwa straika ambao hawajaingia kwenye mfumo wa kufunga mabao.
“Naamini katika mchezo dhidi ya Namungo tutabadilika. Nataka kuona straika wakitengeneza nafasi na kuzitumia. Eneo la beki hakuna tatizo sana kwa kuwa hatujaruhusu wavu kuguswa,” alisema Makata.
Kocha huyo alisema atakaa na nyota wake kujadiliana namna ya kuondokana na matokeo ya sare na badala yake warejeshe makali ya ushindi ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi.
Beki wa timu hiyo, Salum Kimenya alisema licha ya kuanza kwa tabu, lakini bado wana nafasi ya kurejesha heshima na kupata matokeo mazuri akisisitiza kwamba hawakata tamaa.
“Mpira uko hivyo, ila hatujakata tamaa na tunaendelea kujipanga kuhakikisha mechi zilizo mbele yetu tunashinda ukizingatia tumeanzia ugenini na hatujapoteza,” alisema staa huyo.
Msimu uliopita Tanzania Prisons ilimaliza katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.