Mawakili wa Mpina walivyoijibu Serikali kesi aliyomfungulia Spika, Waziri wa Kilimo

Dar es Salaam. Mawakili wa Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina wamejibu hoja za pingamizi la Serikali katika kesi ya Kikatiba aliyoifungua dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na wenzake wawili,  kuwa pingamizi hilo halina mashiko na wakaiomba Mahakama ilitupilie mbali.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba, Mpina anapinga Bunge na utaratibu uliotumika kumpa adhabu ya kumsimamisha kuhudhuria vikao 15 vya Bunge hilo, kwa tuhuma za kusema uwongo dhidi ya Waziri wa Kilimo.

Alipewa adhabu hiyo Juni 24, 2024, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuwasilisha ripoti yake kuhusu tuhuma alizozitoa Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kukiuka sheria katika utoaji wa vibali na uagizaji sukari nje ya nchi.

Kamati hiyo iliyopewa jukumu la kupitia ushahidi wa Mpina katika ripoti yake  ilidai tuhuma za Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo hazikuwa na ukweli, ndipo Bunge chini ya uongozi wa Spika baada ya kujadili likapitisha adhabu hiyo dhidi ya Mpina.

Hata hivyo, Mpina hakukubaliana na uamuzi huo, ndipo akafungua kesi ya Kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge, Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo Mpina anapinga utaratibu uliotumika kumpa adhabu hiyo, akidai uligubikwa na kasoro mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutopewa haki ya kusikilizwa kabla ya kupitishwa uamuzi huo.

Pamoja na nafuu nyingine, pia anaiomba Mahakama hiyo iamuru alipwe stahiki zake kwa kipindi chote atakachokuwa nje ya Bunge.

Hata hivyo, Serikali imemwekea pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikiiomba Mahakama isiikilize.

Katika pingamizi hilo lililosikilizwa jana Jumanne, Septemba 24, 2024, na Jaji Awamu Mbagwa, anayeiwakilisha kesi hiyo, kuanzia saa 4:40 asubuhi mpaka sasa 2:30 usiku, Serikali imetoa sababu tatu kupinga kesi hiyo kusikilizwa.

Katika sababu ya kwanza Serikali ikidai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa Bunge chini ya kanuni zake za kudumu lina mamlaka ya kumsimamisha mbunge, hivyo  lilifanya kilicho ndani ya mamlaka yake.

Sababu ya pili Serikali ikidai alikuwa na nafuu mbadala alizopaswa kuzitumia kwanza kabla ya kufungua kesi ya Kikatiba ambazo ni kuwasilisha kwa Spika malalamiko yake kwa maandishi, au kufungua shauri la mapitio ya Mahakama.

Sababu ya tatu ili Mpina amemuunganisha mdaawa asiyehusika, Waziri wa Kilimo kwani katika kesi hiyo hakuna sababu za madai dhidi wala nafuu ambazo Mpina anaziomba dhidi yake na ikaiomba Mahakama aondolewe katika kesi hiyo.

Wakati wa usikilizwaji huo jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a akishirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kameya na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edwin Webiro.

Mawakili hao wa Serikali wametoa  ufafanuzi wa kina wa sababu hizo za pingamizi lao, huku wakirejea vifungu mbalimbali vya sheria, kanuni za Bunge, Katiba na kesi zilizowahi kuamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Majibu ya mawakili wa Mpina

Wakijibu hoja hizo mawakili wa Mpina, John Seka (kiongozi wa jopo), Ferdinand Makore na Edson Kilatu walipinga vikali hoja za mawakili wa Serikali.

Huku nao wakirejea vifungu vya sheria, kanuni za Bunge, Katiba na kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na mahakama hiyo, Mahakama ya Rufani, wamesisitiza kuwa  ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Seka amesema Kanuni za Kudumu za Bunge zilizonukuliwa na mawakili wa Serikali  zinapaswa kuzingatia sheria na Katiba ya nchi na wakati Bunge linaendesha shughuli zake jambo la kwanza kuzingatia ni Katiba ya nchi.

Seka amesema Ibara ya 89 (1) inaelekeza kuwa Kanuni za Bunge zinazotungwa lazima zizingatie masharti ya Katiba ya Tanzania na Ibara ya 26 (1) ya Katiba inatoa wajibu kwa kila raia na taasisi nchini kuheshimu na kuzingatia Katiba.

“Mheshimiwa inapotokea kukiukwa kwa masharti hayo ya Katiba au haki nyingine za binadamu na milango mingine ikiwa imefungwa, kwa mwananchi wa kawaida jibu si kuandamana bali kuja kugonga milango la Mahakama Kuu.”

Wakili Seka amesema kutokana na hali hiyo ndio maana mteja wao, Mpina ameamua kwenda mahakamani chini ya Ibara ya 108 (2) na 107A (1) ili kutatua changamoto ya kuondolewa bungeni kwa utaratibu usiozingatia masharti ya Katiba, kwani hakuna njia nyingine mbadala.

Wakili Seka amesema  haki zake za Kikatiba anazostahili akiwa bungeni au nje ya Bunge, hazikufuatwa katika mchakato wa kumsimamisha.

Kuhusu nafuu mbadala chini ya kanuni ya 5 (4) ya Kanuni za Bunge, kwamba alipaswa kwenda kulalamika kwa Spika, Wakili Seka amesema siyo sahihi kwani huyohuyo ndiye anayemlalamikia kumshitaki, na ndiye huyohuyo aliyemhukumu, akisisitiza kuwa mahakamani ndiko mahali sahihi.

Pia wakili Seka amesema baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa huku wabunge wakijadili tabia zake, lakini yeye hakupewa haki ya kusikilizwa na hatimaye wakapendekeza adhabu tena walewale waliojadili.

Ameongeza mambo mengine aliyotuhumiwa ameyafanya nje ya Bunge huku akihoji kama kuongea na vyombo vya habari kuhusu kile alichokiwasilisha (ushahidi wake) bungeni ni moja ya mambo yanayolindwa na sheria.

“Kwa hiyo wa kuja kuamua kuwa hili lilifanyika nje ya Bunge ni Mahakama hii,” amesema Wakili Seka.

Wakili Seka pia amesema malalamiko mengine ya mteja wao ni kuitwa muongo wakati anasema alichokisema ni ukweli.

“Kwa hiyo hapa kuna watu wawili, mmoja anasema ni ukweli mwingine anasema ni uwongo. Hivyo kunahitajika mtu ambaye ni independent (asiye na upande) ambaye atasema huu ni uwongo au ni ukweli na mtu huyo ni Mahakama yako,” amesema Seka.

Hivyo Wakili Seka amehitimisha kuwa kinga ya Bunge ina mipaka na kwamba Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kwa upande wake Wakili Makore pamoja na mambo mengine amesema tofauti na Uingereza ambako Bunge ndilo lina  mamlaka ya juu, nchini Tanzania Katiba ndio iko juu ya vyombo vyote.

Kuhusu kuunganishwa Waziri wa Kilimo, Wakili Makore amesema kuwa ingawa hakuna nafuu zozote zinazoombwa dhidi yake. Lakini kwa kuwa ametajwa katika nyaraka na kwamba isingekuwa vema kuendelea bila kumuunganisha ili kumpa nafasi naye ya kusikilizwa.

Kwa upande wake Wakili Edson Kilatu amesema masharti ya kanuni ya 5(4) ya Kanuni za Bunge hayakidhi kuwa nafuu mbadala kwa mteja wao kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika yuleyule anayemlalamikia.

Pia amesema kuwa uamuzi ambao mteja wao anaulalamikia uliridhiwa na Bunge zima na hakuna utaratibu wa kikanuni ulioainishwa kuupinga.

Hivyo amesema katika mazingira ya kesi hiyo hapakuwa na nafuu mbadala ambayo mteja wao angeweza kuifikia.

Kuhusu kufungua shauri la mapitio ya Mahakama amesema kuwa nafuu zinazotolewa katika shauri hilo siyo anaziomba mteja wao, akibainisha kuwa miongoni mwa nafuu anazoziomba ni fidia ambayo haitolewi kwenye shauri la mapitio ya Mahakama.

Wakili Kilatu amesema kuwa ni kupitia shauri hilo tu la Kikatiba chini ya Ibara ya 108 (2) ya Katiba na 107A mteja wao anaweza kupata haki anazoziomba na ambazo haihitaji kutumia kwanza nafuu zilizopo.

Hivyo amesema Ibara hizo mbili ndizo nafuu mbadala pekee na hakuna nyingine.

Jaji Mbagwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 11 , 2024 saa 8 mchana, kwa ajili ya uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali.

Related Posts