Mrithi wa Mgunda Simba huyu hapa

SIMBA Queens inasaka kocha mpya baada ya kuachana na Juma Mgunda na sasa iko mbioni kukamilisha dili la Kocha wa CBE ya Ethiopia, Birhanu Gizaw.

Septemba 8, mwaka huu, Simba Queens ilitangaza kuachana na Mgunda ambaye alidumu katika kikosi hicho kwa msimu mmoja akiipatia timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake na Ngao ya Jamii.

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba katika orodha ya makocha watano ambao Simba imepata wasifu wao (CV), ni Muethiopia Gizaw na mmoja kutoka Nigeria ambaye pia ni mshindani katika nafasi hiyo, lakini uzoefu unamuangusha.

Gizaw siku chache tu zilizopita ametoka kuipa ubingwa wa Cecafa timu CBE ikiifunga Kenya Police Bullets kwa bao 1-0.

Inaelezwa kwamba Simba ipo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha dili la kocha huyo ambaye ana rekodi nzuri kimataifa na ni mzoefu kwenye soka la wanawake kama ambavyo Wekundu wa Msimbazi wanataka.

Hadi sasa mazungumzo baina ya pande mbili yanaonekana kwenda vizuri na inaelezwa Simba itampa mkataba wa mwaka mmoja kwanza ili kumuangalia kocha huyo wa timu za taifa za wasichana U-20 na U-17 za nchini humo.

Rekodi zinaonyesha huyo ndiye kocha aliyesimamia fainali tatu kati ya nne ambazo zimeshuhudiwa misimu tofauti tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo 2021 na msimu huu ikifanikiwa kuchukua ubingwa.

Msimu wa 2021 kocha huyo alitolewa kwenye fainali na Vihiga Queens ila uliofuata ikaishia nusu fainali na She Cooperate ya Uganda ilhali 2023 ilitolewa na JKT Queens kwa penalti 5-4 baada ya suluhu. Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa viongozi wa Simba alisema: “Ni kweli tuna majina matano kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kuna asilimia kubwa (Gizaw) akawa kocha mkuu.”

Related Posts