Mtasingwa kikwazo kwa Mkolombia Azam FC

KIUNGO mkabaji wa Azam FC Mcolombia, Ever Meza amesema yupo sehemu sahihi ndani ya kikosi hicho, licha ya changamoto ya namba kutokana na uwepo wa Adolf Mtasingwa akimtaja kuwa ndiye anampa changamoto kwa sasa kikosini.

Meza ametua Azam FC akitokea Leonnes FC ya kwao Colombia ameliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya kukosa namba ya kudumu kikosi cha kwanza amechagua timu sahihi kwasababu ina mipango endelevu.

“Changamoto niliyokutana nayo Azam ni namba kwenye kikosi cha kwanza kwasababu tayari nimekutana na wachezaji ambao wameonyesha uwezo kama Mtasingwa ni mchezaji mzuri anastahili kucheza,” amesema Meza na kuongeza;

“Mradi uliopo ndani ya Azam na umri nilionao sina sababu ya kuwa na haraka naendelea kujifunza na mimi sikuzote kwenye uchezaji wangu nimekuwa mtu wa kukubali kujifunza hivyo naamini katika kupambana na kuchukua mazuri kutoka anaeaminiwa.” amesema.

Meza amesema pamoja na kukaa nje muda mwingi anaimani kubwa ya kucheza kwenye kikosi hicho kwani anaamini kuwa anakipaji na uwezo mkubwa.

“Pia nafikiri natakiwa kuzoea mazingira ya ligi ili niweze kupewa nafasi ya kucheza nimecheza mchezo mmoja kati ya minne nikianza kikosi cha kwanza dhidi ya JKT Tanzania hivyo nina mwanzo mzuri.” amesema Ever.

Azam hadi sasa imecheza mechi nne za ligi na kiungo huyo ametumika mara moja, huku eneo hilo akicheza zaid James Akaminko, Yanick Bangala na Mtasingwa ambaye amemtaja kuwa ni bora kwake.

Timu hiyo kesho usiku itakuwa wenyeji wa Simba katika pambano jingine la Ligi Kuu linalochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja likiwa pambano la 33 kwa timu hizo katika ligi hiyo tangu 2008.

Related Posts