Kagera. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Igurwa, Adrian Tinchwa (36) kwa tuhuma za kumuua, Phares Buberwa mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Igurwa.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne Septemba 24, 2024 na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Blasius Chatanda imesema mwalimu huyo ambaye ni mkazi wa Kata ya Kanoni wilayani Karagwe, inadaiwa alimshambulia marehemu kwa kumpiga ngumi kwenye paji la uso na kutumia nondo kumpiga nayo miguuni na mikononi baada ya kumtuhumu kuiba simu yake.
“Tukio hili lilitokea Septemba 18, 2024 saa 8:00 mchana katika kijiji cha Kanoni Wilaya ya Karagwe, ambapo mtuhumiwa awali mnamo tarehe hiyo saa 3 asubuhi, imedaiwa alifika nyumbani kwake na kukuta kufuli la mlango wa nyumba yake likiwa limevunjwa na alipotaka kuingia ndani alikutana na Phares Buberwa mlangoni akiwa anatoka ndani huku akijaribu kukimbia,” amesema.
“Na ndipo mtuhumiwa alimkamata na kuanza kumshambulia hadi kusababisha kupata majeraha makubwa mwilini mwake na baadaye mtuhumiwa alimpeleka hadi nyumbani kwa wazazi wake na kumkabidhi kisha wazazi wake walimpeleka katika Kituo cha Afya cha Rwambaizi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu,” amesema Kamanda Chatanda.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa kujichukulia sheria mkononi na kutoa adhabu iliyopitiliza kwa marehemu huyo hadi kufikia hatua ya kukimbizwa kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera linaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu zote zitakapokamilika,” amesema
Chatanda ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake kufuata taratibu na sheria.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera halitasita kuchukua hatua dhidi ya watu wote watakaoshindwa kufuata sheria kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria,” ameongeza.