SAA chache baada ya Biashara United ya Mara kutangaza kuvunja mkataba na kocha mkuu, Henry Mkanwa, imebainika kuwa chanzo cha sakata hilo ni kutakiwa na Pamba Jiji ya Mwanza.
Mkanwa aliyejiunga na Biashara United, Agosti Mosi, mwaka huu, akichukua mikoba iliyoachwa na Amani Josiah aliyetimkia Geita Gold, amedumu kwa siku 52 ndani ya wanajeshi hao wa mpakani.
Kocha huyo wa zamani wa Tabora United ameiongoza Biashara United katika michezo mitatu ikiwemo miwili ya kirafiki dhidi ya Pamba Jiji (0-0) na Singida Black Stars (3-0) na Septemba 22, aliisaidia timu hiyo kushinda mchezo wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu huu wakiichapa Transit Campa bao 1-0.
Leo Septemba 25, 2024 saa 12 jioni Biashara United ilitoa taarifa kwa umma kupitia kurasa za mitandao ya kijamii kuwa imefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha huyo kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili huku ikimtakia mafanikio kwenye majukumu yake mapya.
Mwanaspoti linafahamu kwamba kocha huyo aliwaaga wachezaji na viongozi wa klabu jana Septemba 25 mjini Musoma na kusafiri kwenda jijini Mwanza ambapo alifika jioni (Jumatano) kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Mkanwa anatajwa kuwa kocha msaidizi wa Pamba Jiji kuchukua nafasi ya Salvatory Edward ambaye inaelezwa alikaa pembeni baada ya kutoelewana na Kocha Mkuu, Goran Kopunovic katika mchezo dhidi ya Azam FC, Septemba 14, mwaka huu na kubaki jijini Dar es Salaam.
Mkanwa amelithibitishia Mwanaspoti kumalizana na Biashara United na yupo jijini Mwanza kukutana na Mtanda kumalizia mazungumzo ili asaini mkataba wa kuwa kocha msaidizi wa TP Lindanda.
“Nimeaga asubuhi (Jumatano) kwa sababu Pamba wananihitaji nimeongea na President (Rais wa Biashara United) akakubali basi makubaliano wenyewe (Pamba na Biashara) wanajua walivyokubaliana. Ndiyo nimefika sasa hivi hapa Mwanza nimtafute mkuu wa mkoa kwanza nikimpata tukae chini tuongee ataniambia nianze lini kazi,” amesema Mkanwa